Iran: Diplomasia haikukomesha uwepo wa magaidi Iraq, tumelazimika kuushughulikia kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89214-iran_diplomasia_haikukomesha_uwepo_wa_magaidi_iraq_tumelazimika_kuushughulikia_kijeshi
Ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imemwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo kubainisha hoja na sababu ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya makundi ya kigaidi yaliyoko nchini Iraq na kusisitiza kuwa diplomasia haikuweza kukomesha kuwepo kwa magaidi kaskazini ya nchi hiyo na ndio maana Iran imelazimika kutumia nguvu za kijeshi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 13, 2022 03:17 UTC
  • Iran: Diplomasia haikukomesha uwepo wa magaidi Iraq, tumelazimika kuushughulikia kijeshi

Ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imemwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo kubainisha hoja na sababu ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya makundi ya kigaidi yaliyoko nchini Iraq na kusisitiza kuwa diplomasia haikuweza kukomesha kuwepo kwa magaidi kaskazini ya nchi hiyo na ndio maana Iran imelazimika kutumia nguvu za kijeshi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York imesisitiza kuwa: kwa kutilia maanani hatua haribifu na za uzushaji machafuko za mgenge ya kigaidi dhidi ya wananchi na usalama wa taifa wa Iran na kutokana na kupuuzwa maonyo na malalamiko ya mara kwa mara yaliyotolewa kuhusiana na suala hilo, Tehran haikuwa na chaguo jengine isipokuwa kutumia haki yake na kutoa jibu linalostahiki kwa mashambulio ya kigaidi.
Katika barua yake hiyo kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ofisi ya uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran UN imeashiria hatua za magenge ya kigaidi yenye makao yao kaskazini mwa Iraq na kubainisha hoja na sababu za kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya magenge hayo.
Ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, kuanzia mwaka 2016 hadi sasa tu makundi hayo yamefanya mashambulizi 49 ya kigaidi ndani na karibu na mipaka ya Iran; na matokeo yake watu 24 wameuawa shahidi na wengine 32 wamejeruhiwa na kuongeza kuwa: kwa mujibu wa taarifa za kuaminika, mashambulizi yote hayo ya kigaidi yamepangwa, kuratibiwa na kutekelezwa kutokea eneo la kaskazini mwa Iraq.
Kambi za magaidi zilizoshambuliwa na Iran kwa makombora kaskazini mwa Iraq

Katika barua yake hiyo, ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imebainisha pia kuwa: kwa kutilia maanani vitisho vya kigaidi vinavyoendelea kuwepo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasilisha malalamiko makali tena mara kadhaa kwa kutuma waraka rasmi wa kidiplomasia kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq kuhusiana na kuendelea kuwepo magenge ya kigaidi, kambi zao za mafunzo, harakati yanazoendesha kwa uhuru na vitendo vyao vya uharibifu yanayofanya kutokea ndani ya ardhi ya Iraq.

Barua ya ofisi ya uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran UN imeendelea kueleza kwamba: licha ya malalamiko na maonyo ya mara kwa mara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa masikitiko, mamlaka za eneo la kaskazini mwa Iraq hazikuchukua hatua madhubuti na za maana dhidi ya magaidi kulingana na taratibu za kimataifa.

Katika hali kama hiyo na kwa kutilia maanani mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kufanywa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuwa na chaguo jengine isipokuwa kutumia haki yake ya kujilinda kwa mujibu wa sheria za kimataifa ili kuwahami wananchi wake, usalama wa taifa, mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yake yote.

Ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imetamatisha barua yake hiyo kwa kumtaka Rais wa Baraza la Usalama aiweke barua hiyo kwenye orodha ya nyaraka za baraza hilo.../