Jenerali Qaani: Wamarekani si watu wa uwanja wa vita
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema kuwa mapambano au muqawama ni miongoni mwa kanuni zinazosisitizwa katika dini ya Kiislamu na kusema: "Wamarekani si watu wa medani ya vita na wameshindwa katika medani kuu."
Brigedia Jenerali Ismail Qaani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo jana Jumanne katika kumbukizi ya mwaka wa kwanza wa kuuawa shahidi Hassan Irlu, balozi wa zamani wa Iran nchini Yemen. Katika hotuba yake, amezungumzia muelekeo wa Wamarekani katika miongo miwili iliyopita na juhudi za nchi hiyo za kuunda ulimwengu wenye kuchukua maamuzi ya upande mmoja na kuongeza: "Ili kuvurgua usalama katika eneo, Marekani iliuweka utawala wa Kizayuni wa Israel miongoni mwa mataifa ya Kiislamu."
Jenerali Qaani amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio kitovu cha muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia na kuongeza kuwa: "Mhimili wa muqawama ndio mhimili mkuu wa makabiliano na adui, na katika miaka 20 iliyopita, kwa baraka za uwepo watu kama Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyeuawa shahidi, mhimili huu umeweza kupigana dhidi ya Marekani na utawala huo wa Kizayuni na kupata ushindi."
Hali kadhalika amesema: "Licha ya Wamarekani kutumia dola trilioni saba na makumi ya maelfu ya askari wake waliouawa, hawajapata chochote isipokuwa kudhalilika na taabu tupu."

Maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa kuuawa shahidi Hassan Irlou, balozi wa zamani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Sana'a, mji mkuu wa Yemen, yalifanyika Jumanne jioni mbele ya maafisa wa kijeshi na kiserikali mjini Tehran.
Shahidi Hassan Irlu, ambaye alikuwa mmoja wa maveterani wa vita vya kemikali vya utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Iran, aliambukizwa virusi vya corona akiwa huko Yemen. Kutokana na uzembe wa nchi zilizoivamia Yemen, alichelewa kurejeshwa Iran kupata matibabu na wakati alipowasili nchini hali yake ilikuwa mbaya sana na licha ya jitihada zote za matibabu aliaga shahidi mnamo Desemba 21, 2021.