Iran: Mshikamano wa wananchi wetu umesambaratisha njama za maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i92022-iran_mshikamano_wa_wananchi_wetu_umesambaratisha_njama_za_maadui
Waziri wa Usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mshikamano baina ya watu wa makabila, kaumu na madhehebu tofauti ni fakhari kubwa kwa Iran na kusisitiza kwamba, mshikamano huo ndani ya Iran ya Kiislamu ndio unaosambaratisha njama za maadui.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2022 03:31 UTC
  • Iran: Mshikamano wa wananchi wetu umesambaratisha njama za maadui

Waziri wa Usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mshikamano baina ya watu wa makabila, kaumu na madhehebu tofauti ni fakhari kubwa kwa Iran na kusisitiza kwamba, mshikamano huo ndani ya Iran ya Kiislamu ndio unaosambaratisha njama za maadui.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Hujjatul Islam Sayyid Esmaeil Khatib akisema hayo jana wakati alipotembelea mji wa Orumiyeh katika mkoa wa Azerbaijan Magharibi humu nchini na huku akigusia njama za maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao muda wote wanalenga kuzusha mizozo na fitna kati ya watu wa kaumu, makabila na madhehebu tofauti nchini Iran amesema: Jitihada kubwa na muono wa mbali wa watu wa kaumu tofauti humu nchini, daima umekuwa ukisambaratisha njama za maadui.

Vile vile ameashiria fitna iliyozushwa hivi karibuni na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu katika maeneo tofauti ya Iran na kusema, muono wa mbali na mwamko wa wananchi umezima njama na fitna hiyo ya adui kama ambayo mwamko na jitihada kubwa za vikosi vya Mapinduzi ya Kiislamu na vya kulinda usalama wa taifa, zimesaidia sana kurejea utulivu katika mikoa na maeneo tofauti ya humu nchini. 

Waziri wa Intelijensia wa Iran aidha amesema, maadui wametumia nguvu zao zote za kijasusi na vyombo vyao vya habari na kumwaga fedha nyingi kuchochea machafuko nchini Iran lakini kwa mara nyingine wameshindwa kama walivyoshindwa huko nyuma.

Vile vile amesema: Tehran itaendelea kuwa na mawasiliano mazuri na nchi jirani na itaendelea kuwa amilifu katika mikataba na makubaliano ya kieneo na kimataifa ili kutumia haki yake ya kustafidi ipasavyo na masuala mbalimbali ya ukanda huu na ya kimataifa.