Iran yajibu mapigo, yatangaza vikwazo dhidi ya EU, Uingereza
(last modified Thu, 26 Jan 2023 04:02:29 GMT )
Jan 26, 2023 04:02 UTC
  • Iran yajibu mapigo, yatangaza vikwazo dhidi ya EU, Uingereza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imejibu hatua ya Umoja wa Ulaya na Uingereza ya kuwawekea vikwazo baadhi ya shakhsia binafsi na wa kiserikali wa Jamhuri ya Kiislamu, kwa kutangaza vikwazo dhidi ya shakhsia na taasisi za EU na Uingereza.

Iran imewawekea vikwazo makumi ya maafisa na mashirika ya Umoja wa Ulaya (EU) na Uingereza kutokana na uungaji mkono wao kwa ugaidi na kuchochea ghasia za hivi karibuni hapa nchini.

Baadhi za taasisi za EU zilizowekwa kwenye jalada hilo jeusi la Iran ni pamoja na idhaa ya Radio J ya Ufaransa, Lobi ya Israel katika Bunge la EU inayofahamika kama EFI, na shirika la Bau Heberger kwa kushiriki katika utengenezaji wa viwanda vya kuzalisha silaha za kemikali nchini Iraq, zilizotumika dhidi ya Wairani katika vita vya kulazimishwa vya miaka minane enzi za dikteta Saddam Hussein.

Shakhsia wa Ulaya waliowekewa vikwazo na Iran ni pamoja na Oliver Klein, Waziri wa Masuala ya Miji na Nyumba wa Ufaransa, Dietmar Koster, mwakilishi wa Ujerumani katika Bunge la Ulaya, Timo HEIMBACH, Kamanda vikosi vya Ujerumani nchini Jordan, na Gerad Biard, Mhariri wa jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo, miongoni mwa wengine.

Wengine ni Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa mrengo wa kulia na mwenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu wa Uholanzi na mwenzake wa Sweden, Rasmus Paludan, kwa kuvunjia heshima Qurani Tukufu.

Shakhsia wa Uingereza waliowekwa kwenye orodha hiyo mpya ya vikwazo vya Iran ni Victoria Prentis, Mwanasheria Mkuu wa UK na naibu wake, Michael Tomlinson, Richard Dearlove, aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Kijasusi la MI6, Patrick Sanders, Mkuu wa Majeshi ya Uingereza, na Bethan David, Mkuu wa Kitendo cha Kupambana na Ugaidi cha UK, pamoja wengine.

Bunge la EU karibuni lilitangaza kuliweka jeshi la IRGC la Iran katika orodha ya 'ugaidi'

Januari 23, Baraza la Ulaya liliongeza shakhsia na taasisi 37 za Kiirani; na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ikaongeza majina saba ya shakhsia na taasisi saba za Iran kwenye vikwazo vyao.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inalinda haki yake ya kujibu mapigo kwa Umoja wa Ulaya na utawala wa Uingereza na kwamba, hatua ya EU na UK ni ishara ya kudumaa kiakili kwa kushindwa kumaizi ukweli halisi kuhusu Iran, na vilevile ni matokeo ya mkanganyo uliowapata kutokana na nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Alisema hatua hizo ni ishara ya kulemewa, kufadhaika na kukasirika kutokana na namna walivyoshindwa kifedheha hivi karibuni kuvuruga uthabiti na utulivu nchini Iran licha ya kila juhudi walizofanya na kutumia gharama kubwa.

Tags