Shambulio 'butu' lililogonga mwamba dhidi ya kituo cha kijeshi cha Esfahan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93470-shambulio_'butu'_lililogonga_mwamba_dhidi_ya_kituo_cha_kijeshi_cha_esfahan
Wizara ya Ulinzi ya Iran ilitangaza usiku wa kuamkia jana Jumapili kuwa, jengo moja la karakana za Wizara ya Ulinzi mjini Esfahan lililengwa na shambulio lililofeli la ndege tatu ndogo zisizo na rubani aina ya Micro Air Vehicle (MAV), ambapo moja ya droni hizo ilitunguliwa, nyingine ilinaswa kwenye mtego wa mitambo ya ulinzi wa anga na droni tatu iliangukia kwenye paa la karakana hiyo na kuripuka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 30, 2023 04:53 UTC
  • Shambulio 'butu' lililogonga mwamba dhidi ya kituo cha kijeshi cha Esfahan

Wizara ya Ulinzi ya Iran ilitangaza usiku wa kuamkia jana Jumapili kuwa, jengo moja la karakana za Wizara ya Ulinzi mjini Esfahan lililengwa na shambulio lililofeli la ndege tatu ndogo zisizo na rubani aina ya Micro Air Vehicle (MAV), ambapo moja ya droni hizo ilitunguliwa, nyingine ilinaswa kwenye mtego wa mitambo ya ulinzi wa anga na droni tatu iliangukia kwenye paa la karakana hiyo na kuripuka.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Iran baada ya kutokea mripuko katika kiwanda kimoja cha sekta ya ulinzi mjini Esfahan imeelezwa kuwa: shambulio hilo lililofeli lilitokea Jumamosi usiku, lakini hujuma hiyo ya ndege ndogo zisizo na rubani ilizimwa kwa mafanikio kutokana na tahadhari zilizokuwa zimechukuliwa na mikakati iliyotekelezwa na kitengo cha mitambo ya ulinzi wa anga.
Micro Air Vehicle (MAV)

Japokuwa hayajatolewa maelezo zaidi kuhusiana na shambulio hilo butu Jumamosi usiku, lakini mashambulio kama hayo yameshatokea huko nyuma, ambapo miripuko kadhaa imewahi kujiri kandokando ya vituo vya kijeshi na vya nyuklia vya Iran.

Katika mashambulio na hujuma zote hizo za uharibifu, maadui wamejaribu kutumia kila njia ili kuzuia na kukwamisha maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sekta ya ulinzi na nyuklia na pia kuilazimisha Iran ichukue hatua za kuwaridhisha maadui hao na kulegeza misimamo katika sera zake za ulinzi.
Ukweli ni kwamba maadui, wakiwemo Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, wanaotekeleza sera za kuzidisha mashinikizo na kuitenga Iran, katika miaka ya karibuni wametumia kila mbinu, kuanzia mauaji ya kigaidi mpaka hujuma za uharibifu ili kusimamisha kikamilifu au kuichelewesha miradi ya ulinzi na ya nyuklia ya Iran. Mashambulio ya utegaji mabomu, hujuma za kimtandao na mauaji ya makamanda wa Muqawama na wanasayansi wa nyuklia wa Iran ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na maadui kwa lengo la kuweka vigingi na vizuizi katika njia ya maendeleo ya kisayansi na kiulinzi, na kwa madhumuni ya kupunguza uwezo na nguvu zinazoongezeka na kuimarika zaidi kila uchao za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Nembo la Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Kwa kutoa mfano, baada ya kuuawa mwanasayansi wa nyuklia wa Iran, Mohsen Fakhrizadeh mnamo mwezi Novemba 2020, gazeti la Independent la Uingereza liliandika wakati huo katika moja ya makala zake za uchambuzi kuwa: mauaji kadhaa ya hivi karibuni nchini Iran ni sehemu ya hatua zisizo na kikomo za mfumo wa ujasusi wa Israel kwa kushirikiana na wenzake wa nchi za Magharibi, ikiwemo MI6 na CIA, zenye lengo la kuvuruga au kuchelewesha, na ikiwezekana, kuizuia Iran isifanikishe kusudio lake la kufikia malengo yake ya nyuklia.

Ni dhahiri kuwa licha ya hatua na jinai zote ambazo maadui wamezifanya kwa lengo la kutoa pigo na kuudhuru uwezo na nguvu za kiulinzi na za nyuklia za Iran, hawajaweza kuvuruga chochote katika mipango ya Tehran, hasa ya kujitosheleza katika mifumo muhimu ya zana za kijeshi na mitambo ya ulinzi; na hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inahesabiwa kuwa moja ya nchi zinazoongoza duniani katika sekta mbalimbali za kijeshi kama vile makombora yenye shabaha kali, ndege zisizo na rubani na mitambo ya ulinzi.
Mashirika adui ya ujasusi ya Marekani (CIA), Uingereza (MI6) na Israel (Mossad)

Kwa kuzingatia hilo, Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetamka kuwa, inalihakikishia taifa adhimu la Iran ya Kiislamu kwamba, vituo vya ulinzi vya taifa hili vitaendeleza kwa kasi na uzito mkubwa hatua zake za kuimarisha nguvu, uwezo, amani na usalama na kusisitiza kwamba hatua hizo 'butu' za hujuma za maadui hazitakuwa na athari yoyote hasi kwa maendeleo na ustawi wa nchi../