Vurugu uchaguzi mdogo Kenya zaibua wasiwasi kuelekea uchaguzi mkuu 2027
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139970-vurugu_uchaguzi_mdogo_kenya_zaibua_wasiwasi_kuelekea_uchaguzi_mkuu_2027
Mashambulio dhidi ya wapiga kura wakati wa uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Ol Kalou katika mkoa wa kati nchini Kenya, yameibua hofu kuhusu hali ya usalama kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwakani 2027.
(last modified 2026-07-18T03:32:02+00:00 )
Jul 18, 2026 03:30 UTC
  • Vurugu zatawala uchaguzi mdogo OI Kalou, Kenya
    Vurugu zatawala uchaguzi mdogo OI Kalou, Kenya

Mashambulio dhidi ya wapiga kura wakati wa uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Ol Kalou katika mkoa wa kati nchini Kenya, yameibua hofu kuhusu hali ya usalama kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwakani 2027.

Watu waliokuwa na silaha walivamia vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi huo ukiendelea, wakirusha mabomu ya machozi na kuwashambulia wapiga kura.

Magari ya raia yalionekana yakiwa na watu wenye silaha huku wakiwatisha wananchi kuacha kupiga kura katika uchaguzi huo ambao mgombea wa upinzani Sammy Waweru kutoka chama cha DCP, amemshinda Muchina Nyaga kutoka chama tawala cha UDA kwa kura zaidi ya 35,000 na kutangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi.

Uchaguzi huu mdogo kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, ulikuwa kama kipimo cha ushawishi wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya kati ya rais William Ruto na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua.

Aidha, wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa hali vurugu iliyoonekana Ol Kalou inaweza kuwa mbaya zaidi katika maeneo mengine ya nchi, wakati huu rais William Ruto anapotafuta muhula wa pili wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika mwezi Agosti mwaka 2027.

Uchaguzi huo uliandaliwa kumsaka mrithi wa marehemu David Kiaraho ambaye aliaga dunia mnamo Machi mwaka huu.

Akihutubu kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa mshindi, Sammy Waweru Mbunge mteuule kutoka chama cha DCP alilaani ghasia zilizodaiwa kusababishwa na wahuni wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi siku ya Alhamisi, hali iliyovuruga upigaji kura katika vituo vingi vya kupigia kura ndani ya mji wa Ol Kalou.