Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini Venezuela
Akiwa ziarani nchini Venezuela, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini ambapo amekuwa pia na mashauriano na Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro.
Katika mazungumzo hayo, Hossein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria safari ya Rais Nicolas Maduro mjini Tehran na kusainiwa hati ya ushirikiano wa pamoja kama nukta kuu katika uhusiano wa pande mbili, na kulitaja suala la kutekelezwa haraka mapatano hayo ya pande mbili ili kuimarisha ushirikiano kuwa hatua muhimu.
Huko nyuma pia yaani mwezi Juni mwaka jana Marais wa Iran na Venezuela walisaini hapa mjini Tehran hati ya ushirikiano wa pamoja wa kimkakati wa miaka 20 kati ya nchi mbili hizo. Hati hiyo inajumuisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Iran na Venezuela katika nyanja za kielimu, kiutamaduni, kiutalii, kiuchumi, kinishati, kiviwanda na kibiashara kati ya nchi mbili. Kutiwa saini hati hiyo ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Iran na Venezuela kunaonyesha utangamano na kurandana siasa za nje za Tehran na Caracas hususan katika kukabiliana na vikwazo na hatua za upande mmoja za serikali ya Marekani.
Nchi za Amerika ya Latini zimezingatiwa pakubwa katika fremu ya doktrini ya sera za nje za Iran; na serikali ya 13 ya Iran kwa kuzingatia shaari za sera zake za nje zenye uwiano huku serikali hiyo ikifanya juhudi za kuimarisha na kuboresha uhusiano na majirani zake na nchi za kanda hii imetangaza kuwa: inataka kumarisha uhusiano na nchi waitifaki katika maeneo mbalimbali zikiwemo nchi za Amerika ya Latini. Viongozi wa nchi hizo zikiwemo Venezuela, Cuba na Nicaragua pia mara kadhaa wameeleza matarajio yao ya kupanua uhusiano wa serikali zao na Iran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Venezuela ambazo zinahesabiwa kuwa wamiliki wakubwa wa akiba ya mafuta na wazalishaji wa mafuta, katika miongo kadhaa iliyopita zimekuwa chini ya mashinikizo ya kiuchumi ya upande mmoja na yasiyo ya kiadilifu. Vikwazo dhidi ya nchi mbili hizi vimepunguza chanzo kikuu cha fedha za kigeni na mapato ya nchi hizo yaani mauzo yao ya mafuta kulikoathiriwa na vikwazo hivyo tajwa.
Pamoja na hayo yote, Iran na Venezuela zimedumisha uhusiano wao katika nyanja za viwanda na sayansi; na katika miaka ya karibuni nchi mbili zimetilia mkazo juu ya ulazima wa kuungwa mkono maamuzi ya pande kadhaa ili kulinda maslahi yao ya pamoja mkabala wa hatua na misimamo ya upande mmoja ya Marekani.
Wakati huo huo tunapasa kutilia maanani kwamba, uchumi wa Iran na Venezuela unaweza kutumiwa na pande mbili kukamilishana; kwa mfano Venezuela inahitajia bidhaa zinazozalishwa na wataalamu wa ndani, bidhaa za petrokemikali, kilimo na vifaa na suhula mbalimbali za ujenzi ambapo Venezuela inaweza kudhaminiwa aghalabu ya bidhaa hizo kwa kushirikiana makampuni ya Kiirani na Venezuela. Katika upande mwingine Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inakabiliwa na baadhi ya majanga ya kimaumbile kama ukame; na uwepo wa ardhi yenye rutuba huko Venezuela ni fursa pia kwa ajili ya makampuni ya kilimo ya Kiirani kufanya shughuli za kilimo nje ya nchi. Ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikataka kuzidishwa kiwango cha ushirikiano kati yake na nchi za Amerika ya Latini ikiwemo Venezuela kwa kuzingatia fursa mbalimbali zilizopo katika eneo hilo.
Wakati huo huo Iran na Venezeula zinaendelea kushirikiana kwa pamoja katika nyanja za nishati, ujenzi wa mitambo ya nishati ya joto, ukarabati wa mitambo ya kusafisha mafuta ya Venezuela, katika huduma za kiufundi na uhandisi, sekta ya kiuchumi, kilimo na ulinzi. Ziara za mara kwa mara za viongozi wa nchi mbili hizi pia zinathibitisha ukweli huu kwamba uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Iran na Venezuela utaimarika na kupanuka zaidi. Kuhusiana na suala hilo, Rais wa Venezuela ameitaja ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini humo kuwa fursa nzuri kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa pande mbili na kueleza kuwa: "tunapasa kuanza mwaka mpya kwa nguvu na uwezo mkubwa na kufuatilia kwa nguvu miradi ya ushirikiano."