"Wamagharibi wanalia machozi ya mamba kuwahadaa wanafunzi, wazazi wa Iran"
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewakosoa maafisa wa nchi za Magharibi ambao wanaiahadaa dunia kwa kuonesha kuwa wameguswa na kutiwa wasiwasi na matukio ya wanafunzi wa kike wa Jamhuri ya Kiislamu kudaiwa kushambuliwa kwa gesi ya sumu wakiwa shuleni na kusisitiza kuwa, kilio hicho cha Wamagharibi ni sawa na machozi ya mamba.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, radiamali za Wamagharibi kwa suala hilo ni sehemu ya vita mseto vya maadui wa taifa hili la Kiislamu.
Sanjari na kusema kuwa vyombo husika vya Iran vinachunguza na kuifuatilia kadhia hiyo, amesisitiza kuwa wananchi wa Iran wanafahamu vyema hadaa, unafiki na machozi ya mamba ya maadui ambao wanaendelea kuiwekea nchi hii vikwazo vya kikatili.
Wakati huo huo, Nasser Kana'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amezikosoa vikali nchi hizo za Magharibi kwa kujaribu kutumia suala hilo kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema Iran inafuatilia suala hilo na tayari washukiwa kadhaa wametiwa mbaroni. Kadhalika amewataka Wamagharibi kujiepusha na mchezo wao mchafu wa kisiasa kwa kutumia kadhia hiyo na madai ya kujikariri ya kukiukwa haki za binadamu hapa nchini.
Hapo jana, Rais Ebrahim Raisi alizungumzia pia vita hivyo vya kipropaganda vya adui vyenye lengo la kueneza chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzusha hofu na unyonge katika nyoyo za wanafunzi na familia zao humu nchini.
Amesisitiza kuwa, ametoa amri kwa Waziri wa Usalama wa Taifa na Waziri wa Mambo ya Ndani kufuatilia haraka na kutoa ripoti kamili kuhusu matukio ya hivi karibuni katika skuli za baadhi ya miji humu nchini ambapo hali za kiafya za baadhi ya wanafunzi ziliharibika wakiwa shuleni.