Rais Raisi asisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa Iran na Iraq
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa Iran na Iraq katika nyuga tofauti.
Rais Raisi alitoa mwito huo jana Jumatano katika mazungumzo ya simu na Mohammed Shia' Al Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq na kueleza kuwa, nchi mbili hizi jirani zina fursa na uwezo wa kuboresha ushirikiano wao katika nyuga za nishati, biashara, viwanda, fedha na benki.
Kadhalika Rais wa Iran amemnyooshea mkono wa pongezi, kheri na fanaka Waziri Mkuu wa Iraq kwa mnasaba wa maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (AF).
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hiyo jana iliungana na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Imam wa mwisho wa madhehebu ya Shia, Mahdi (AF).
Rais wa Iran amesema mataifa haya mawili yana uhusiano wa karibu na wa kihistoria, ambao mizizi yake ni utamaduni, ustaarabu na dini zinazofanana.
Kadhalika Sayyid Raisi amegusia ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na Iraq hasa kwa kurejelea hati za ushirikiano zilizosainiwa na mataifa haya mawili katika safari ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa Iraq hapa Tehran.
Kwa upande wake, Mohammed Shia' Al Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq amempongeza Rais wa Iran kwa mnasaba wa maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa Imam Mahdi (AF), mwana wa Imam Hasan al Askari (AS) ambaye alizaliwa mjini Samarrah Iraq mwezi 15 Shaaban mwaka 255 Hijria.
Al Sudani amesema serikali na wananchi wa Iraq wanawashukuru ndugu zao Wairani kwa misaada yao hasusan katika vipindi vigumu lililokabiliwa navyo taifa hilo la Kiarabu.