Iran yakanusha kufikia 'makubaliano ya muda' na Marekani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali ripoti kwamba Iran na Marekani zinafikia "makubaliano ya muda" ambayo yatapelekea kuondolewa vikwazo kwa Jamhuri ya Kiislamu mkabala wa kufanyika mabadiliko katika mpango wa amani wa kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini.
Shirika la Habari la Iran (IRNA) limenukuu taarifa ya mwakilishu wa Jamhuri ya Kiislamu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa ikisema: Hakuna makubaliano ya muda ya kuchukua nafasi ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kwamba suala hilo haliko katika ajenda.
Awali tovuti ya Middle East Eye (MEE), ikinukuu vyanzo viwili ambavyo haikutaja majina yao, ilidai kuwa Iran na Marekani zinakaribia kufikia makubaliano ya muda ya kuondoa baadhi ya vikwazo mkabala wa kubanwa shughuli za kurutubisha madini ya uranium nchini Iran.
Alhamisi iliyopita pia, msemaji wa Baraza la Usalama waTaifa la Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, alikanusha ripoti ya MEE, akiitaja kuwa ya uongo na ya kupotosha.
Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalifikiwa mwaka 2015 kati ya Iran na nchi kubwa duniani ikiwemo Marekani. Makubaliano hayo yalipunguza vikwazo kwa Jamhuri ya Kiislamu, ambayo kwa upande wake, ilijitolea kupunguza baadhi ya shughuli zake katika sekta ya uzalishaji wa nishati ya nyuklia.
Hata hivyo, Marekani ilijiondoa katika makubaliano hayo mwaka 2018 chini ya uongozi wa rais wa zamani, Donald Trump, na kurudisha vikwazo vyote ambavyo makubaliano hayo yalikuwa yamevindoa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa iwapo upande wa Marekani utachukua hatua kwa kutilia maanani uhalisia na ukweli wa mambo, kuna uwezekano wa kufikia makubaliano.