Ebrahim Raisi: Iran imetimiza vigezo vyote vya kuwa mwanachama wa BRICS
Rais Ebrahim Raisi amezungumzia uhusiano wa Iran na Jumuiya ya Shanghai na Jumuiya ya Eurasia pamoja na maandalizi yake mazuri ya kuwa mwanachama katika kundi la BRICS na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imetimiza vigezo vyote na tuna matumaini ya kukubaliwa kuwa wanachama wa kundi hilo la BRICS.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana jioni mjini Tabriz na kuongeza kuwa, leo Iran imo kwenye masoko ya dunia kiasi kwamba viongozi wa ngazi za juu wa baadhi ya nchi wameiomba rasmi Jamhuri ya Kiislamu iwauzie bidhaa zake nyingi.
Aidha amesema: Ukuaji wa uchumi wa Iran unatokana na kukua na kuongezeka uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha amesema kuwa, ushirikiano na nchi za kigeni ni sehemu muhimu sana katika ukuaji wa uchumi, lakini miundombinu pia ni muhimu sana.
Vile vile amesisitiza kuwa, kuna wajibu wa kujiepusha na mambo yanayoweza kuwakatisha tamaa wawekezaji na kuongeza kuwa, kuandaa miundombinu yenye uwezo wa kuvutia wawekezaji na kujenga hali ya usalama na utulivu pamoja na kumdhaminia faida mwekezaji ni katika mambo ya dharura ya ustawi wa kiuchumi.
Amesema, rasilimali watu iliyo nayo Iran leo hii ni kubwa hasa miongoni mwa vijana, lakini lazima nguvu kazi hiyo iwezeshwe, ielimishwe na irahisishiwe njia za kuingia kwenye gurudumu la uzalishaji, vinginevyo itakuwa ni nguvukazi na rasilimali watu hiyo kuingia kwenye mtego wa udalali.