Kiongozi Muadhamu: Sekta ya nyuklia ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumapili ameonana na wanasayansi, wataalamu na wabobezi wa masuala ya nyuklia wa Iran na kusisitiza kuwa, sekta ya nyuklia ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa maisha ya wananchi wetu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo na kusisitiza kuwa, sekta ya nyuklia ni muhimu kwa maendeleo na uwezo wa Iran katika masuala ya ufundi, uchumi, matibabu na mengineyo kwa ajili ya ustawi wa wananchi wetu. Vile vile ni muhimu katika upande wa siasa za kieneo na kimataifa.
Amesema, kufanywa teknolojia ya nyuklia kuwa ya ndani ya Iran ni jambo muhimu sana na ni pigo kwa Magharibi na kwa watu wenye fira za Kimagharibi ambao wanafanya njama za kulidhalilisha taifa na kudhoofisha moyo wao kufanya kazi na kuishi kwa matumaini mazuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, maadui hawataki kabisa kuona taifa la Iran linapiga hatua za maendeleo na ndiyo sababu kuu inayowafanya waisakame sana Iran katika kadhia yake ya nyuklia.
Amesisitiza kuwa, sekta hiyo ndio ufunguo wa maendeleo makubwa ya nchi na taifa katika nyuga tofauti kama ambavyo pia maadui wanaogopa sana kuona mataifa mengine yanaifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa kigezo chao cha ustawi na maendeleo.
Aidha amesema, pande zinazohusika na masuala ya nyuklia ukiwemo wakala wa IAEA kwa miaka mingi zimetoa ahadi za kila namna kwa taifa la Iran lakini hazijatekeleza ahadi zao na hili linathibitisha wazi kuwa, hatuwezi kuwa na imani na ahadi za pande hizo.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, silaha za mauaji ya umati, ziwe za nyuklia au za kemimali; zinapingwa na dini tukufu ya Kiislamu na lau kama msingi huo wa Uislamu usingekuwepo na kama sisi tungeamua kuzalisha silaha za nyuklia, tungekuwa tumeshafanya hivyo zamani na maadui wanajua kuwa wasingeweza kutuzuia.