Rais wa Iran aanza safari ya kuzitembelea nchi za Amerika ya Latini
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja uhusiano wa Iran na nchi huru za Amerika ya Latini kuwa wa kistratijia.
Rais Ebrahim Raisi ameyasema hayo mapema leo kabla ya kuondoka nchini akielekea Venezuela, katika hatua ya kwanza ya safari yake kwenye nchi kadhaa za Amerika ya Latini.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, safari hii inafanyaka kwa mwaliko rasmi wa marais wa Venezuela, Nicaragua na Cuba na kusema kuwa, leo hii aghalabu ya nchi za eneo la Amerika ya Kusini ni nchi zinazotaka kuishi kwa uhuru na kujitawala, na kwamba moyo wa kupigania uhuru, kujitawala na mapambano dhidi ya ubeberu ni sifa ya pamoja ya nchi za eneo hilo zenye uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akiashiria kuwa Iran imekuwa na uhusiano mzuri na Venezuela, Nicaragua na Cuba katika miaka iliyopita, Raisi ameongeza kuwa, mbali na uhusiano wa kirafiki wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara na nchi hizo, Iran pia inashirikiana na nchi hizo katika uga wa nishati, na katika miaka 2 iliyopita, uhusiano katika nyanja za viwanda, kilimo, sayansi na teknolojia, na dawa na tiba umestawi kwa njia ya kuridhisha baina ya Tehran na nchi hizo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametaja uuzaji nje wa huduma za kiufundi na uhandisi kuwa ni maeneo mengine ya ushirikiano kati ya Iran, Venezuela, Nicaragua na Cuba na ameeleza matumaini yake kwamba, kwa kuzingatia sera ya kuimarisha uhusiano na nchi jirani, rafiki na zenye mwelekeo sawa ya serikali ya awamu ya 13, hapana shaka kuwa mashauriano na utiaji saini wa mikataba wakati wa safari hizo utakuwa hatua na madhubuti ya kuboresha kiwango cha uhusiano na nchi hizi 3 katika eneo la Amerika ya Kusini.