Raisi: Marekani inawaua mashujaa wa kupambana na ugaidi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Marekani ilitaka kusimamisha gurudumu la maendeleo ya taifa la Iran kwa kutumia vikwazo na vitisho, lakini taifa la Iran limetumia vitisho na vikwazo hivyo kama fursa ya maendeleo.
Sayyid Ebrahim Raisi ameyasema hayo baada ya kuwasili Managua nchini Nicaragua mapema leo Jumatano kwa lengo la kustawisha na kuimarisha uhusiano wa pande mbili baada ya kukamilisha safari yake nchini Venezuela.
Baada ya hafla ya kumkaribisha rasmi iliyotayarishwa na mwenyeji wake, Daniel Ortega, Rais wa Nicaragua, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehutubia kundi la vijana wa nchi hiyo, akiashiria kusadifiana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Mapinduzi ya Nikaragua na taathira za mapinduzi haya mawili, na amewapongeza mashujaa wa kitaifa wa mapambano dhidi ya ubeberu katika nchi zote mbili.
Sayyid Ebrahim Raisi amesema kupigania uhuru na uadilifu ni sifa za pamoja za mapinduzi ya wananchi wa Iran na Nicaragua na kuongeza kuwa, Iran iko tayari kustawisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote hususan katika uga wa sayansi na teknolojia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyataja madai ya eti kutetea demokrasia na haki za binadamu yanayotolewa na Wamagharibi kuwa ni uongo na kusema kuwa, Wamagharibi hususan Wamarekani wanapaswa kuheshimu tawala zinazotokana na kura za watu, lakini wanafanya kinyume.
Akizungumzia nafasi na mchango wa Wamarekani katika kuunda kundi la kigaidi la ISIS, na vilevile sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kupambana na ugaidi, Ebrahim Raisi amesema: Wanadai kuwa wanpambana na ugaidi, lakini walimuua shahidi shujaa wa mapambano dhidi ya ugaidi, Haj Qassem Soleimani.
Kwa upande wake, Daniel Ortega, Rais wa Nicaragua amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na yale ya watu wa Nicaragua yalikuwa na misingi imara katika mapambano dhidi ya tawala za kibeberu hususan Marekani ambayo daima hufanya mikakati ya kulazimisha matakwa yake kwa nchi nyingine.
Rais wa Nicaragua amewasifu mashujaa wa kitaifa wa nchi mbili hizo, na amelaani jinai ya Wamarekani ya kumuua kigaidi Haj Qassem Soleimani. Vilevile ameagiza kukaa kimya kwa dakika moja kwa ajili ya kutoa heshima kwa shujaa Muirani wa mapambano dhidi ya ugaidi, Jenerali Soleimani.