AI: Myanmar inapaswa kuchunguza mashambulizi ya msikiti
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i9949-ai_myanmar_inapaswa_kuchunguza_mashambulizi_ya_msikiti
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeyataja mashambulizi yaliyofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wa Myanmar dhidi ya msikiti kuwa ni jinai na kusisitiza kuwa, machafuko mapya yanayolenga Waislamu nchini humo yanapaswa kufuatiliwa na wahusika wake kuadhibiwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 25, 2016 14:36 UTC
  • AI: Myanmar inapaswa kuchunguza mashambulizi ya msikiti

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeyataja mashambulizi yaliyofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wa Myanmar dhidi ya msikiti kuwa ni jinai na kusisitiza kuwa, machafuko mapya yanayolenga Waislamu nchini humo yanapaswa kufuatiliwa na wahusika wake kuadhibiwa.

Amnesty imeitaka serikali ya Myanmar ichukue hatua za haraka na kufanya uchunguzi wa kuwasaka wahusika wa mashambulizi hayo.

Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Kusini Mashariki mwa Asia na Pacific, Rafendi Djamin amesema tukio hilo linapaswa kuchunguzwa haraka na kwa uhuru kamili na washukiwa wafikishwe kwenye vyombo vya sharia. Amesisitiza kuwa, wahanga wa mashambulizi hayo pia wanapaswa kupewa fidia.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeitahadharisha serikali ya Myanmar kwamba kutotekelezwa uadilifu katika suala hilo itakuwa ishara ya kupuuzwa mashambulizi yanayofanywa dhidi ya wafuasi wa dini za wachache.

Ijumaa ya jana kundi la Mabudha 200 wenye misimamo mikali lilishambulia msikiti wa Waislamu katika kijiji cha Thuye Tha Mein katika mkoa wa Bago na kuharibu msikiti huo. Vilevile wakazi wa eneo hilo walilazimika kukimbilia katika kituo cha polisi kwa kuhofia usalama wao.

Machafuko hayo yalianza baada ya kutokea mzozo juu ya ujenzi wa shule ya Waislamu katika eneo hilo.

Maelfu ya Waislamu wa Myanmar wameuawa na wengine wengi kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi yanayofanywa na mabudha wenye misimamo mikali.