Abdollahian aitaka Ulaya ikabaliane na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka Ulaya ichukue hatua za maana na athirifu kwa ajili ya kukabiliana na aina kwa aina ya vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu.
Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Josep Borrell, Mkuu wa Sera Kigeni wa Umoja wa Ulaya ambapo mbali na kujadiliana naye kuhusiana na matukio ya hivi karibuni kieneo na kimataifa wawili hao wamebadilishana mawazo kuhusiana na uhusiano wa Iran na Ulaya.
Abdollahian amesisitiza katika mazungumzo yake na Borrell juu ya ulazima wa Ulaya kuchukua hatua za maana na athirifu kwa ajili ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na hatua ya hivi karibuni ya kuvunjiwa heshima Qur'ani tukufu huko nchini Sweden.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amezungumzia matukio ya Ukraine na kueleza kwamba, daima Jamhurii ya Kiislamu ya Iran imekuwa muungaji mkono wa amani na uthabiti uliimwenguni ikiwemo Ukraine na kwamba, inaamini kuwa, usitishaji vita unawezekana tu kupitia ubunifu wa kisiasa.

Kwa upande, Josep Borrell, Mkuu wa Sera Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, kuvunjiwa heshima Qur'ani tukufu, siyo msimamo wa Umoja wa Ulaya na kwamba, umoja huo unalaani kitendo chochote kile na uvunjiaji heshima wa aina yoyote ile dhidi ya dini.
Jumatano iliyopita ya tarehe 28 mwezi Juni raia mmoja wa Sweden alichoma moto na kuchana nakala ya Qur'ani Tukufu huko Stockholm. Kabla ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu, Momika aliweka nyama ya nguruwe kwenye nakala ya kitabu hicho kitukufu, ambayo ni ishara ya kukidunisha na kukivunjia heshima kupitiliza kwa waumini wa dini ya Kiislamu.