Iran:Kuanzishwa ujumbe wa UN kuhusu machafuko ya mwaka jana 'kumechochewa kisiasa'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99590-iran_kuanzishwa_ujumbe_wa_un_kuhusu_machafuko_ya_mwaka_jana_'kumechochewa_kisiasa'
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha ripoti ya ujumbe uliopewa mamlaka na Umoja wa Mataifa kuhusu machafuko ya mwaka 2022 nchini, ikisema hatua ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa ya kuanzisha ujumbe kama huo ilichukuliwa kwa malengo ya kisiasa na haikubaliki".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2023 04:36 UTC
  • Iran:Kuanzishwa ujumbe wa UN kuhusu machafuko ya mwaka jana 'kumechochewa kisiasa'

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha ripoti ya ujumbe uliopewa mamlaka na Umoja wa Mataifa kuhusu machafuko ya mwaka 2022 nchini, ikisema hatua ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa ya kuanzisha ujumbe kama huo ilichukuliwa kwa malengo ya kisiasa na haikubaliki".

Kazem Gharibabadi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran aliyasema hayo jana Jumatano katika kikao cha 53 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kufuatia ripoti ya kile kinachojulikana kama ujumbe wa kutafuta ukweli kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Iran katika ghasia zilizozuka nchini Septemba mwaka jana.

Ripoti hiyo iliishutumu Iran kwa kutoa "adhabu kali" kwa watu wanaoshukiwa kuhusika na "maandamano makubwa," ikitoa wito kwa nchi Tehran kusitisha hukumu ya kunyongwa wale waliohukumiwa kifo kutokana na ghasia hizo na kuwaachilia wale wote waliozuiliwa.

Akijibu ripoti hiyo, Gharibabadi amesema kuanzishwa kwa utaratibu huo, licha ya Iran kuwajibika ipasavyo wakati na baada ya ghasia hizo, kunaonyesha siasa za kinafiki na undumakuwili.

Amesema, nchi zilizochochea ghasia nchini Iran na baadaye zikanaswa katika hali kama hiyo ya ghasia na fujo, ndizo zilizoanzisha utaratibu huo wa kuhoji haki za binadamu nchini Iran.

Gharibabadi amesema kilichotokea Iran mwaka jana si mikusanyiko na maandamano ya amani, bali zilikuwa ghasia na mashambulizi ya kigaidi yaliyochochewa na makundi ya kisiasa ya Magharibi na kutekelezwa kwa msaada wa kifedha, silaha na vyombo vya habari vya mashirika ya usalama ya nchi za Magharibi.

"Nchi kadhaa za Magharibi zilihusika katika kuchochea ghasia hizo. Magaidi pia waliingia katika matukio hayo na karibu watu 100 wenye mafungamano na makundi ya kigaidi, wengi wao wakiwa wafuasi wa kundi la MKO, walikamatwa," alisema.

Afisa huyo alisema mtandao wa kijamii wa Instagram wenye makao yake nchini Marekani uliruhusu watumiaji kuwafundisha watu jinsi ya kutengeneza mabomu, na katika Twitter zaidi ya watumiaji 50,000 bandia wa lugha ya Kiajemi waliundwa katika mwezi wa kwanza wa maandamano ili kueneza propaganda chafu dhidi ya Iran.

Ameongeza kuwa, vituo vya televisheni vya London, ikiwa ni pamoja na BBC Persian na Iran International, vilitenga sehemu kubwa ya programu zao kuchochea ghasia na kuwapa magaidi jukwaa dhidii ya Iran.

Gharibabadi amesisitiza kuwa mataifa ya Magharibi hayako katika nafasi ya kuzungumzia haki za wanawake na watoto nchini Iran, wakati wao wenyewe wanakiuka haki za wanawake na watoto katika nchi zao.