Iran yamwita mwanadiplomasia wa Uingereza kuhusu matamshi ya uingiliaji ya London
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemwita balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran kuwasilishiwa malalamiko kuhusu matamshi "haribifu na uingiliaji" ya balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Isabelle Marsh aliitwa na mkurugenzi mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia masuala ya Ulaya Magharibi siku ya Alhamisi, kwa sababu balozi wa Uingereza mjini Tehran hayupo, saa chache baada ya Barbara Woodward, balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa kulihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) ambapo amekosoa mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.
Woodward aliishutumu Iran kuwa eti imekiuka Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linaloidhinisha Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA), makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na madola sita makubwa duniani mwaka 2015.
Marekani ilitupilia mbali mkataba huo mwaka 2018 na kurejesha vikwazo ambavyo ilikuwa imeviondoa. Huku wakisalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani, washirika wa Magharibi wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa na Ujerimani walijiunga na vikwazo vya Marekani kwa karibu na kusitisha hughuli zao za kibiashara na Tehran.
Woodward alikashifu mfululizo wa hatua za kulipiza kisasi ambazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikizichukua kulipiza kisasi, bila kutaja ukiukaji wa nchi za Magharibi wa mapatano hayo ambao umesababisha kulipiza kisasi kwa Jamhuri ya Kiislamu. Iran imesema itabadilisha tu hatua yake ya kulipiza kisasi ikiwa madola ya Magharibi yatarejelea ahadi yao ya JCPOA.

Pia aliishutumu Iran kwa kupatia Russia ndege zisizo na Rubani, madai ambayo Tehran imeyakanusha mara kwa mara sambamba na kupinga vita ambavyo vimekuwa vikiendelea nchini Ukraine.
Wakati alipoitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana Alhamisi, balozi mdogo wa Uingereza alifahamishwa kuhusu malalmiko ya Iran kufuatia matamshi wa Woodward.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameitaka serikali ya Uingereza "ijiepusha kuingia kwenye mitego ambayo imewekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na makundi ya kigaidi."
Afisa huyo alikuwa akiashiria kuhusu propaganda za chuki dhidi ya Iran ambazo zimekuwa zikienezwa na Israel na kundi la kigaidi la MKO ambazo zinalenga kuchafua jina la Jamhuri ya Kiislamu duniani.
Mkurugenzi mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia masuala ya Ulaya Magharibi amemfahamisha balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran kwamba, "iwapo Uingereza itaendelea na mbinu ya uharibifu basi hilo ni jambo ambalo Iran kamwe haitalikubali na bila shaka litakabiliwa na hatua sawia za Jamhuri ya Kiislamu."
Isabelle Marsh amesema atafikisha malamiko hayo ya Iran kwa serikali ya Uingereza.