China yataka vikwazo dhidi ya Iran viondolewe na Magharibi iheshimu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99658-china_yataka_vikwazo_dhidi_ya_iran_viondolewe_na_magharibi_iheshimu_jcpoa
Naibu Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amezitaka nchi za Magharibi ziheshimu na zitekeleze kikamilifu vipengee vya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuindolea Iran vikwazo vyote ilivyowekewa kidhulma baada ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jul 07, 2023 23:55 UTC
  • China yataka vikwazo dhidi ya Iran viondolewe na Magharibi iheshimu JCPOA

Naibu Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amezitaka nchi za Magharibi ziheshimu na zitekeleze kikamilifu vipengee vya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuindolea Iran vikwazo vyote ilivyowekewa kidhulma baada ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, Geng Shuang amesema hayo kujibu njama za nchi za Ulaya za kuendelea na vikwazo vya silaha na makombora dhidi ya Iran na kusema mjini Washington kwamba, nchi za Magharibi zinapaswa kuheshimu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama na kuiondolea Iran vikwazo vyote kama ilivyokubaliwa katika mapatano ya JCPOA.

Wiki iliyopita, vyombo vya habari vya Magharibi vilisambaza vipoti na kutangaza kuwa nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa kushirikiana na Marekani zina nia ya kurefusha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya makombora ya Iran. Vikwazo hivyo vinamaliza muda wake mwezi Oktoba mwaka huu.

 

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amejibu njama hizo za nchi za Magharibi akisema kuwa, nchi za Ulaya na Marekani zinapaswa kujifunza kutokana na makosa yao ya huko nyuma na zisiendelee na siasa zao hizo za kiuadui dhidi ya Iran.

Wakati huo huo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amejibu swali kuhusu tamko lililo dhidi ya Iran lililotolewa na nchi hizo tatu za Ulaya na kusema kuwa, azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama kuhusiana na makubaliano ya JCPOA lazima liheshimiwe na kutekelezwa kikamilifu na pande zote.

Hata mwakilishi wa Ulaya ameunga mkono mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kutaka kufanyike juhudi za kidiplomasia za kuanza kuheshimiwa vipengee vya makubaliano hayo.