Mashauriano ya kirafiki yanayotawala katika uhusiano wa Iran na Algeria
(last modified Sun, 09 Jul 2023 08:23:33 GMT )
Jul 09, 2023 08:23 UTC
  • Mashauriano ya kirafiki yanayotawala katika uhusiano wa Iran na Algeria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Ahmed Attaf, ambaye amekuwa ziarani hapa nchini kwa mwaliko wa Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ametoa matamshi ya kirafiki na ya heshima sana kuhusu uhusiano wa Algeria na Iran katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari aliofanya na mwenyeji wake.

Ahmad Attaf aliwasili nchini jana Jumamosi na kulakiwa na  Amir-Abdollahian katika makao ya Wizara ya Mambo ya Nje; na baada ya kikao na majadiliano ya baina ya pande mbili alihudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari. Jambo lililotoa mguso katika matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria ni upendo na heshima ambayo nchi yake inaipa Iran. Attaf aliitaja mara kadhaa Iran kuwa nchi rafiki na ndugu; na mbali na kueleza alivyofurahia kuwepo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mapokezi makubwa aliyopewa yeye na ujumbe wake, alisema: “Ni kama kwamba tuko katika nchi yetu wenyewe". Aidha ameuelezea uhusiano wa Iran na Algeria kuwa ni mzuri sana na kusisitiza juu ya nia na irada thabiti waliyonayo marais wa nchi mbili ya kustawisha uhusiano huo.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Algeria katika mkutano na waandishi wa habari

 

Kuna mambo kadhaa ya mtazamo wa pamoja katika sera za nje za Iran na Algeria. Nchi zote mbili ni waungaji mkono wa kweli na wa dhati wa Palestina, ambapo Algeria ni nchi iliyopinga utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika. Aidha, Tehran na Algiers zimekuwa na msimamo mmoja kuhusu ulazima wa kuheshimiwa mamlaka ya utawala ya Syria; na Algeria, kama ilivyo Iran, imekaribisha kurejeshwa uhusiano wa nchi za Kiarabu na Syria na kurejea Damascus kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Kuhusiana na hilo, katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Algeria, Hossein Amir-Abdollahian amesema, "leo tulikuwa na mazungumzo juu ya masuala ya kikanda. Algeria haikuruhusu utawala wa Kizayuni uwe mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika. Nchi hii daima imekuwa ikiunga mkono Palestina na imetoa mchango muhimu kuhusiana na kurejea Syria kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria (kushoto) alipoonana kwa mazungumzo na Rais Ebrahim Raisi (kulia)

 

Suala jengine muhimu katika uhusiano wa Iran na Algeria ni ushirikiano wa pamoja wa nchi hizo mbili katika taasisi za kieneo na kimataifa, ambapo tunaweza kuashiria hapa uungaji mkono wa Iran kwa Algeria kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na juhudi za pamoja za nchi hizo mbili za kujiunga na BRICS.
 
Nukta nyingine muhimu ni kuhusu uhusiano wa pande mbili katika nyuga zingine zisizokuwa za sera ya nje. Licha ya ukweli kwamba Iran na Algeria zina uhusiano imara wa kisiasa, kuna kiwango kidogo mno cha biashara zinazofanywa kati ya nchi hizi mbili. Uuzaji wa bidhaa za Algeria kwa Iran ni wa kiwango cha chini mno na bidhaa za Iran zilizouzwa kwa Algeria katika mwaka uliopita zilikuwa takribani dola milioni 100 tu. Katika miongo miwili iliyopita, Iran imekuwa ikisafirisha bidhaa zake za jadi kuelekea Algeria yakiwemo matunda yaliyokaushwa kama zabibu kavu na pistashio, lakini katika miaka ya karibuni, Tehran imekuwa ikiiuzia chuma pia Algiers. Wakati wa ziara ya Ahmad Attaf mjini Tehran, umetiliwa mkazo ulazima wa kustawishwa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili. Kuhusiana na hilo, Amir-Abdollahian amesema, "Leo, tumekubaliana kuongeza kasi zaidi ya ushirikiano kati ya pande mbili katika nyanja za sayansi, teknolojia, makampuni ya kitaaluma, kilimo, dawa, vifaa tiba, viwanda na madini." Kuondolewa viza ya kisiasa kati ya nchi mbili kupitia makubaliano yaliyofikiwa hapo jana, kunaweza pia kuandaa mazingira ya kupanuliwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Algeria na Iran.../