Iran: Marekani inafanya hima kurefusha vita vya Ukraine
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mpango wa Marekani wa kutuma nchini Ukraine mabomu 'yaliyopigwa marufuku ya vishada na kusisitiza kuwa, Washington inafanya kila iwezalo ili kuhakikisha kuwa vita vya Ukraine havimaliziki haraka.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akisema hayo katika ujumbe aliotuma leo Jumapili kwenye mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa, Marekani kutuma mabomu ya vishada nchini Ukraine kunaonesha namna Washington ilivyojitolewa kwa dhati kuufanya mgogoro wa Ukraine kuwa mpana zaidi.
Ijumaa ya juzi, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Jake Sullivan alithibitisha kuwa Washington imeazimia kutuma silaha hizo haramu nchini Ukraine ndani ya siku chache zijazo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hatua ya US kutuma silaha hizo haramu Ukraine ni mfano mwingine wa wazi unaoonyesha hulka ya kupenda kuvuruga uthabiti ya Marekani, na kwamba hakuna shaka mpango huo utashadidisha umwagikaji wa damu na uharibifu zaidi.
Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Vishada ulianza kutekelezwa mwaka 2010, na tayari nchi zaidi ya 100 duniani zimesaini mkataba huo.

Hii ni katika hali ambayo, waitifaki wa Marekani katika Shirika la kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), zikiwemo Uingereza, Canada na Uhispania zimepinga mpango huo wa Washington wa kutuma silaha hizo haramu nchini Ukraine. Aidha Russia na Umoja wa Matafa zimekosoa mpango huo wa Marekani wa kutuma silaha haramu za vishada nchini Ukraine.
Shirika la kutetea kaki za binadamu la Human Rights Watch hivi karibuni lilitangaza kuwa, lina ushahidi mpya unaoonyesha kuwa jeshi la Ukraine linatumia mabomu ya kutega ardhini yaliyopigwa marufuku dhidi ya raia.