Amir-Abdollahian: Kusitasita na kuchelewa kulaani kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu ni undumilakuwili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99816-amir_abdollahian_kusitasita_na_kuchelewa_kulaani_kuvunjiwa_heshima_qur’ani_tukufu_ni_undumilakuwili
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, kusitasita na kuchelewa kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu ni ishara ya undumakuwili na misimamo ya nyuso mbili.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jul 12, 2023 03:53 UTC
  • Amir-Abdollahian: Kusitasita na kuchelewa kulaani kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu ni undumilakuwili

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, kusitasita na kuchelewa kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu ni ishara ya undumakuwili na misimamo ya nyuso mbili.

Shirika la Habari la Fars limeripoti habari hiyo na kumnukuu Hossein Amir-Abdollahian akisema hayo jana Jumanne, Julai 20, mbele ya kikao cha 53 cha Baraza la Haki za Binadamu kuhusu mada ya dharura ya "ongezeko la kutisha la vitendo vya makusudi vya chuki na kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini mjini Geneva Uswisi na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakuhesabu kufanyika kikao hicho hivi sasa kuwa ni jambo la dharura, na ni jambo la lazima, muhimu na lililofanyika kwa wakati mwafaka ndani ya baraza hilo.

Ameongeza kuwa: Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden hivi karibuni, ambalo ni tukio la sita ya aina hiyo katika nchi za Ulaya Magharibi kwa mwaka huu wa 2023, ni kitendo kinachochochea waziwazi ghasia, chuki, ubaguzi na uadui dhidi ya Waislamu.

Kibaraka wa MOSSAD akilindwa na jeshi la polisi la Sweden ili achome moto nakala ya Qur'ani Tukufu

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesisitiza kuwa, kuchoma moto Qur'ani Tukufu si tu ni ukiukaji wa haki za binadamu, bali pia ni ukiukaji wa haki za Waislamu zaidi ya bilioni 2 duniani. Vitendo hivyo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya watu wengine lazima vilaaniwe mara moja na watetezi wote wa haki za binadamu.

Amesema: Ni lazima mianya yote ya kisheria katika ngazi ya kitaifa na kimataifa iondolewa, ili kuzuia kurudiwa kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu haraka iwezekanavyo.

Amesema: Tunaisisitizia sana serikali ya Sweden na nchi nyingine za Ulaya kuwachukulia hatua za haraka na madhubuti wahusika wa vitendo hivyo vya kuudhi na vya kuchukiza ili kuzuia visitokee tena katika siku za usoni.