Kan'ani: Magharibi yafumbia macho maandamano makubwa ya Israel, yatia chumvi kwingineko
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99984-kan'ani_magharibi_yafumbia_macho_maandamano_makubwa_ya_israel_yatia_chumvi_kwingineko
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amevilaumu vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuhusu upotoshaji wao wakati wa kuripoti maandamano makubwa huko Israel, akisema maandamano katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu yanakuja huku vyombo hivyo hivyo vya habari vikizidisha chumvi wakati wa kuripoti machafuko kwingineko duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 16, 2023 08:57 UTC
  • Kan'ani: Magharibi yafumbia macho maandamano makubwa ya Israel, yatia  chumvi kwingineko

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amevilaumu vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuhusu upotoshaji wao wakati wa kuripoti maandamano makubwa huko Israel, akisema maandamano katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu yanakuja huku vyombo hivyo hivyo vya habari vikizidisha chumvi wakati wa kuripoti machafuko kwingineko duniani.

Nasser Kan'ani aliandika katika ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumapili kwamba,"Tunashuhudia mwendelezo wa maandamano ya miezi kadhaa, migomo na maandamano ya kulemaza yanayohudhuriwa na mamia ya maelfu ya watu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel)."
Amesema maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) hukabiliwa na ukandamizaji na ukatili, na idadi kamili ya waliouawa, kujeruhiwa na kukamatwa mikononi mwa vikosi vya usalama na polisi wa utawala wa Kizayuni bado haijulikani.
Aidha amesema, "mfumo wa  vyombo vya habari vya Magharibi, hufumbia macho ukandamizaji na unyanyasaji dhidi ya waandamanaji sambamba na kudunisha mauaji na ukandamizaji wa Wapalestina unaofanywa na Wazayuni." Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema vyombo vya habari vya Magharibi hujaribu kuonyesha maandamano kama hayo kama ishara ya demokrasia katika hali ambayo ni wazi kuwa hakuna demokrasia yoyote Israel.

Maandamano dhidi ya Netanyahu huko Tel Aviv

Kan'ani amesema kuwa wakati vyombo hivyo hivyo vya habari vinaangazia kwa mapana mikusanyiko na maandamano madogo madogo katika nchi isiyofungamana na nchi za Magharibi,  huyatangaza kuwa ya vurugu, uharibifu na mapinduzi.

Maandamano yameshadidi tena katika utawala haramu wa Israel baada ya bunge kupitisha kifungu muhimu cha mpango wa utawala huo wa kufanya mageuzi katika mfumo wa mahakama, ambayo wapinzani wanasema yanatishia kile kinachodaiwa kuwa eti ni demokrasia katika utawala huo.

Serikali yenye misimamo mikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imeendeleza hatua hiyo yenye utata licha ya maandamano makubwa tangu kupendekezwa kwa mageuzi hayo mwezi Januari.

Machafuko na maandamano ya sasa huko Israel yamepelekea kuongezeka maonyo kuhusu uwezekano wa kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa Wazayuni wanaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.