Sep 28, 2023 14:17 UTC
  • Kamanda wa jeshi la Iraq: Hatuhitaji wanajeshi wa kigeni wawepo nchini

Kamanda wa operesheni za pamoja za vikosi vya ulinzi vya Iraq amesema: "nchi hii ina uwezo unaohitajika wa kupambana na magaidi na wala haihitaji kuwepo askari wa kigeni".

Licha ya kufanyika duru kadhaa za mazungumzo ya kimkakati kati ya Iraq na Marekani kwa ajili ya kuhitimisha kuwepo kijeshi Marekani nchini Iraq kutokana na kumalizika kwa vita vya kupambana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS); na licha ya kuidhinishwa pia mpango wa kuwatimua wanajeshi wote wa kigeni katika ardhi ya Iraq katika bunge la nchi hiyo, Marekani ingali inahalifu kutekeleza mpango huo kwa kuendelea kuwepo katika ardhi ya Iraq.
 
Kwa mujibu wa kanali ya habari ya Al-Ahad, Tahsin al-Khafaji, kamanda wa operesheni za pamoja za vikosi vya ulinzi vya Iraq ameeleza kwamba, vikosi vya kijeshi vya Iraq vimepiga hatua na vina uwezo unaohitajika wa kukabiliana na magaidi wa DAESH.
Askari wa jeshi vamizi la Marekani wakiranda katika mitaa ya Iraq

Al-Khafaji amesisitiza kuwa: vikosi vya kijeshi vya Iraq vina utayari wa kijeshi wa kiwango cha juu na vimepata mafanikio ya kuridhisha katika mipaka yote ya nchi hiyo.

 
Kamanda wa operesheni za pamoja za vikosi vya ulinzi vya Iraq amebainisha kuwa: usalama wa mipaka ni jukumu la walinzi wa mpakani na vikosi hivyo vina uwezo na nyenzo zinazohitajika ili kudhamini usalama wa Iraqi nzima.
 
Al-Khafaji ameongeza kuwa: Jeshi na vikosi vya usalama vilivyo chini ya harakati ya Hashd al-Shaabi ya Iraq vinazuia makundi ya kigaidi kujipenyeza ndani ya nchi na vinafuatilia kwa karibu harakati zote za magaidi hao.
 
Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Shia al-Sudani amesisitiza mara kadhaa kwamba hakuna haja ya vikosi vya muungano wa kimataifa wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kuwepo katika ardhi ya nchi hiyo.
 
Aidha, Al-Sudani amesema: kundi la kigaidi la ISIS sasa si tishio tena kwa nchi hiyo na hakuna haja ya kuwepo muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani ambao uliundwa kwa ajili ya kukabiliana na kundi hilo.../

 

Tags