Feb 24, 2024 06:18 UTC
  • Ehud Olmet: Lengo la Netanyahu ni kuwapora Waislamu Msikiti wa Al Aqsa

Waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni amefichua kuwa, Ghaza ni hatua ya mwanzo tu ya baraza la vita la Benjamin Netanyahu kwani lengo lao kuu ni kuwafukuza Wapalestina wote, huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kuwapokonya Waislamu Msikiti wa al Aqsa na kuziingiza ardhi hizo ndani ya maeneo mengine yaliyopachikwa jina la Israel.

Gazeti la al Quds al Arabi limeripoti habari hiyo na kumnukuu Ehud Olmet  akisema jana kwenye makala iliyochapishwa na gazeti la Kizayuni la Haaretz kwamba baraza la mawaziri la Netanyahu ni genge la wahalifu.

Amesema, lengo kuu la pande mbili zenye misimamo mikali yaani Itmar bin Gvir na waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayauni  si kuishia Ukanda wa Ghaza tu, bali ni kuwafukuza Wapalestina katika maeneo yao yote. 

Ehud Olmet

 

Waziri mkuu huyo wa zamani wa Israel ameongeza kuwa, hata ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye maeneo wanayoporwa Wapalestina na mashambulizi ya maangamizi dhidi ya Ghaza si lengo kuu la genge lenye ndoto ambalo limehodhi madaraka ya utawala wa Kizayuni hivi sasa.

Wakati huohuo, Usama Hamdan, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa HAMAS amesema kuwa, kama si Marekani, basi leo hii Wapalestina wasingeliendelea kuteseka kwa njaa huko Ghaza na wala wasingeliendelea kuuawa kwa umati. 

Amesema hayo usiku wa kumakia leo Jumamosi na kuongeza kuwa, wote wanaoshiriki kwenye jinai zinazoendelea kufanywa na Wazayuni wana dhima kubwa na kwamba kuendelea mateso ya wananchi wa Ghaza ni ushahidi kwamba madola ya kibeberu hasa Marekani yamempa amri Netanyahu ya kuendelea kufanya jinai bila ya huruma huko Palestina hasa kwenye Ukanda wa Ghaza.