Feb 26, 2024 07:15 UTC
  • Kuendelezwa mauaji ya halaiki ya jeshi la Israel  katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza

Wapalestina wengine wameuawa shahidi kufuatia mashambulizi ya anga na mizinga ya jeshi katili la Israel linaloendeleza mauaji ya kimabari katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Kanali ya Habari ya Quds, Wapalestina 10 waliuawa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa Jumapili katika shambulizi la wanajeshi wa Israel kwenye nyumba moja katika eneo la al Zeitoun katika mji wa Gaza.

Wapalestina wengine wawili pia waliuawa shahidi katika shambulio la helikopta za utawala wa Kizayuni mashariki mwa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Katika muktadha huo, Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, katika jinai mpya 7 zilizotekelezwa Jumapili utawala haramu wa Kizayuni umeua Wapalestina  86  na kuwajeruhi wengine 131.

Maiti za Wapalestina

Kanali ya Televisheni ya Al Jazeera pia imechapisha picha za shambulio la anga la Israel kwenye nyumba moja katikati ya Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, lililopelekea Wapalestina 8 kuuawa shahidi.

Kanali hiyo ya Televisheni pia imechapisha picha za shambulio la kombora la utawala wa Kizayuni katika nyumba moja katika eneo la Al-Shaimaa huko Beit Lahia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kusababisha moto mkali ambapo idadi kadhaa ya Wapalestina wameuawa shahidi na kujeruhiwa.

Kanali ya Telegram ya Shams News pia imechapisha picha za kuondolewa miili ya mashahidi waliokuwa wamenaswa chini ya kifusi cha nyumba ambayo awali ililengwa na kuharibiwa na utawala ghasibu wa Israel katika eneo la Al-Shaimaa lililoko katika mji wa Beit Lahia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya mashahidi katika Ukanda wa Gaza imeongezeka hadi 29,692 na  waliojeruhiwa ni 69,879.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, baadhi ya mashahidi na wahanga bado wako chini ya vifusi mitaani, na utawala wa Kizayuni unawazuia waokoaji kuchukuliwa hatua yoyote kuhusiana na jambo hilo.

Machungu ya Wapalestina

Nibal Farsakh, Msemaji wa Hilali Nyekundu ya Palestina huku akielezea hali ya kusisitiza  ya Ukanda wa Gaza  na kuwa wakaazi wake wote wanakabiliwa na utapiamlo ameongeza kwamba maelfu ya watu wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya Israel.

Habari nyingine ni kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wamewazuia waumini wa Kipalestina kuingia katika Msikiti wa Al-Aqswa kwa kuchukua hatua kali za kiusalama na kijeshi katika milango na vitongoji vinavyouzunguka, ambapo baadhi ya walowezi wa Kizayuni wameushambulia msikiti huo kwa uungaji mkono wa vikosi uvamizi vya Al-Quds.

Klabu ya Wafungwa wa Kipalestina imetangaza kuwa, katika masaa  machache yaliyopita, wanajeshi wa Kizayuni wanaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu wamewatia mbaroni Wapalestina wengine 15 akiwemo mwandishi wa habari na baadhi ya watu walioachiwa huru, kufutia mashambulizi yaliyofanywa katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

 

Tags