Apr 20, 2024 02:59 UTC
  • OIC yalaani hatua ya Marekani kuzuia azma ya Palestina kuwa mwanachama kamili wa UN

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani hatua ya Marekani ya kuzuia ombi la Palestina la kutaka uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa, huku Israel ikiendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza kwa msaada wa baadhi ya nchi za Magharibi hususan Marekani.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imeeleza masikitiko yake makubwa kutokana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kuipa Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa, huku taifa la Palestina likikabiliwa na ukatili mkubwa zaidi, mateso na mauaji ya kimbari,” OIC ilisema katika taarifa yake iliyotolewa jana Ijumaa.

Taarifa ya OIC imesisitiza kuwa: "Kura ya veto ya Marekani dhidi ya rasimu ya azimio ilipendekeza kuipa Palestina uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, "inakiuka masharti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaoruhusu uanachama kwa nchi zote zinazokubali majukumu yaliyomo katika mkataba huo."

OIC imesisitiza kwamba hatua ya Marekani inawazuia watu wa Palestina kupata "haki zao halali", na "inachangia kurefusha ukandamizaji wa kihistoria" ulioanzishwa dhidi ya watu wa Palestina kwa miaka 75.

OIC imezipongeza nchi zilizopiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio hilo, ikisema msimamo huo "unaonyesha uungaji mkono wao kwa ukweli, haki, uhuru na amani na kukataa kwao sera" za utawala wa Israel.

Katika upigaji kura huo, nchi 12 wanachama wa Baraza la Usalama la UN zilipiga kura za kuunga mkono, Uswisi na Uingereza zilipiga kura ya kutopinga au kuunga mkono upande wowote; na Marekani imezuia kupitishwa azimio hilo kwa kulipigia kura ya veto.

Tags