Apr 29, 2024 11:03 UTC
  • UNRWA: Takriban watoto 17,000 wametenganishwa na familia  zao Gaza kufuatia vita vya Israeli

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limebainisha wasiwasi wake juu ya hali inayozidi kuzorota ya watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, huku Israel ikiendeleza vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo linalozingirwa.

Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili, UNRWA ilisema watoto wanakabiliwa na maisha yaliyosambaratika huko Gaza, na kuongeza kuwa kwa uchache watoto 17,000 katika eneo hilo linalozingirwa wametanganishwa na familia zao.

Mbali na hayo Phillipe Lazzarini, kamishna mkuu wa UNRWA, amesema kuongezeka kwa joto huko Gaza kumesababisha vifo vya watoto wasiopungua wawili.

Joto kali linaloendelea, limeathiri zaidi ya watu milioni mbili wanaoishi katika hali mbaya katika Ukanda wa Gaza, na kusababisha vifo vingi, ikiwa ni pamoja na vya watoto.

Ripoti kadhaa za vyombo vya habari zinasema halijoto imepanda karibu nyuzi joto 30 katika siku za hivi karibuni, juu ya hali ya kawaida, wakati huu wa mwaka.

UNRWA imebainisha zaidi kuwa hali ya maisha huko Gaza inazidi kuwa mbaya huku hali ya joto ikiongezeka, ikisisitiza kwamba watoto wanalipa gharama kubwa zaidi huku ikikariri wito wake wa kusitishwa mapigano mara moja.

Utawala haramu wa Israel umekuwa ukiwalenga watoto kwa makusudi vitani Gaza na takwimu zinaoneyesha kuwa aghalabu ya Wapalestina zaidi ya 34,000 waliouawa vitani Gaza ni wanawake na watoto.