Apr 29, 2024 11:19 UTC
  • Wanajeshi 14 wa Israel waangamizwa, wajeruhiwa katika operesheni ya muqawama Gaza

Takriban wanajeshi watatu wa utawala katili wa Israel wameangamizwa na wengine 11 kujruhiwa vibaya katika eneo la vita kati kati mwa Ukanda wa Gaza, huku vikosi vya muqawama au mapambano ya Kiisalmu Palestina vikiendelea kulisababishia hasara kubwa jeshi katili la utawala huo.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba wanajeshi watatu wa akiba waliouawa walikuwa wanachama wa Kitengo cha 99 cha Jeshi la Israel. Walipoteza maisha yao karibu na kituo cha ukaguzi cha Netzarim, kinachotenganisha kaskazini na kusini mwa Gaza. Wanajeshi wengine kumi na moja wa Israel wamejeruhiwa vibaya katika operesheni hiyo.

Ripoti zinasema kwamba baadhi ya wanajeshi wa Israel waliondolewa kwa helikopta, huku wengine wakiendelea kutibiwa katika eneo la tukio.

Kikosi cha Brigedi za Izzedin al-Qassam, tawi la kijeshi la kundi la kupigania ukombozi wa Palestina Hamas, kimetangaza kuwa kimelenga kituo cha jeshi la Israel huko Netzarim kwa makombora mazito.

Wapiganaji  wa Kikosi cha Brigedi za Izzedin al-Qassam

Jeshi la Israel hadi sasa limethibitisha vifo vya takriban askari 260 kati ya wanajeshi wake tangu kuanzisha uvamizi wa nchi kavu huko Gaza. Idadi ya askari wa Israel walioangamizwa katika vita hivyo inaaminika kuwa zaidi ya hiyo.

Wakati huo huo, askari 30 wa akiba wa kikosi cha mwavuli cha Israel wamekataa kuitikia mwito wa kushiriki katika shambulio tarajiwa la nchi kavu dhidi ya Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza kwa kuhofia maisha yao.

Israel ilianzisha vita dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina kutekeleza operesheni ya kushtukiza ya kulipiza kisasi jinai za miaka mingi za Israel.

Hadi sasa utawala katili wa Israel umeua Wapalestina wasiopungua 34,454 wa Gaza, wengi wao wakiwa ni wanawake, watoto na vijana.