May 02, 2024 02:36 UTC
  • Utawala wa Kizayuni umewatia nguvuni mamia ya wafanyakazi wa Kipalestina

Vyanzo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa Wazayuni maghasibu wamewatia mbaroni zaidi ya wafanyakazi elfu tano wa Kipalestina katika mwaka huu wa 2024 huku hali za kiafya za raia hao wa Kipalestina zikitajwa kuwa mbaya.

Shirika la habari la Shahab  jana liliripoti kuwa Muungano wa Kitaifa wa Wafanyakazi wa Palestina umetangaza katika taarifa yake kuwa: Katika mwaka huu 2024, jeshi la Israel liliwatia nguvuni wafanyakazi 5,100 wa Kipalestina katika maeneo yao ya kazi huko Ukanda wa Gaza au wakati walipokuwa wakirejea katika eneo hilo. 

Kamatakamata ya Israel dhidi ya wafanyakazi wa Kipalestina 

Taarifa ya Muungano wa Kitaifa wa Wafanyakazi wa Palestina imeongeza kuwa: Zaidi ya wafanyakazi 235,000 wa Kipalestina katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu wameacha kufanya kazi tangu miezi sita iliyopita. 

Hii ni katika hali ambayo, Klabu ya Kuwahami Mateka wa Kipalestina ilitangaza siku tatu zilizopita kuwa utawala wa Kizayuni tokea Oktoba 7 mwaka jana na sambamba na kuanza oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa umewatia nguvuni Wapalesina 8,505 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.  

Utawala wa Kizayuni umewafuta kazi  wafanyakazi wengi wa Kipalestina tangu tarehe 7 Oktoba 2023. 

Wafanyakazi wa Kipalestina waliofukuzwa kutoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu hadi Gaza wameeleza kuwa Wazayuni waliwavua nguo, waliwatesa, waliwafunga kwenye vizimba na kuwapiga vikali.