May 02, 2024 11:46 UTC
  • Baada ya uamuzi wa kihistoria wa Colombia; Hamas yataka mataifa yote kuvunja uhusiano na Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imepongeza na kukaribisha kwa mikono miwili uamuzi wa Colombia wa kuvunja uhusiano wake na utawala haramu wa Israel.

Hamas mbali na kukaribisha uamuzi huo, imetoa mwito kwa mataifa yote ya dunia kuvunja uhusiano wao na utawala huo ghasibu unaofanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza kwa karibu miezi saba sasa.

 Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeeleza kuwa, uamuzi wa Colombia ni "ushindi kwa kujitolea muhanga watu wetu.

Rais Gustavo Petro, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Israel huko Gaza, alitangaza uamuzi huo jana alipohutubia maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) katika mji mkuu wa nchi hiyo Bogota.

Akitangaza uamuzi huo, Rais wa Colombia alisema: "Na sisi hapa mbele yenu, serikali ya mabadiliko, Rais wa Jamhuri anataarifu kwamba kesho (Alkhamisi) uhusiano wa kidiplomasia" na utawala wa Israel "utakatwa".

Mnamo mwezi Oktoba 2023 pia, Rais wa Columbia alimshambulia vikali waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni Yoav Gallant kwa kutumia lugha dhidi ya watu wa Gaza ambayo alisema ni sawa na waliyoitumia Wanazi kuhusu Wayahudi. Utawala wa Kizayuni uliamua "kusimamisha usafirishaji wa vifaa vya masuala ya usalama" kwa nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.

Wapalestina wasiopungua 34,568 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana wameshauawa shahidi hadi sasa katika vita vya kinyama vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni tarehe 7 Oktoba kufuatia operesheni ya ulipizaji kisasi ya Kimbunga cha Al-Aqswa iliyotekelezwa na makundi ya Muqawama ya Gaza.