Mazungumzo ya Iran na Umoja wa Ulaya na fursa zilizopo
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i19225-mazungumzo_ya_iran_na_umoja_wa_ulaya_na_fursa_zilizopo
Maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya wamekutana mjini Brussels Ubelgiji na kufanya mazungumzo kuhusiana na mambo muhimu yanayolihusu eneo la Mashariki ya Kati pamoja na masuala ya pande mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2016 23:52 UTC
  • Mazungumzo ya Iran na Umoja wa Ulaya na fursa zilizopo

Maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya wamekutana mjini Brussels Ubelgiji na kufanya mazungumzo kuhusiana na mambo muhimu yanayolihusu eneo la Mashariki ya Kati pamoja na masuala ya pande mbili.

Kikao hicho kimefanyika kwa uongozi wa pamoja wa Helga Schmid Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na Majid Takht-Ravanchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa mara ya kwanza Iran na Umoja wa Ulaya zilifanya kikao cha pande mbili mwezi Februari mwaka huu mjini Tehran. Jumatano ya juzi, Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa mwishoni mwa kikao hicho cha pande mbili ukieleza kuwa, katika kikao cha Brussels kulijadailiwa uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Iran katika baadhi ya mambo yakiwemo ya biashara, nishati, mazingira, uhamiaji, elimu, utamaduni, utafiti wa kielimu na usafiri na uchukuzi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pande mbili zilijadili na kubadilishana mawzo pia kuhusiana na masuala ya Mashariki ya Kati, hususan hali ya mambo nchini Syria, Iraq, Yemen, Lebanon na Afghanistan. Kadhalika maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya walizungumzia pia suala la haki za binadamu.

Helga Schmid na Majid Takht-Ravanchi

Helga Schmid Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na Majid Takht-Ravanchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran walifanya kikao kwa nyakati tofauti kilichohudhuriwa na wawakilishi wa Benki Kuu ya Iran na Kamishna wa Ulaya kwa ajili ya kuchunguza masuala ya kiuchumi, kifedha na kibenki. Kikao hicho kimefanyika katika hali ambayo, matokeo ya urais wa Marekani na kuibuka na ushindi Donald Trump  yamewashangaza wengi ukiwemo Umoja wa Ulaya. 

Kwa kuzingatia matamshi aliyokuwa akiyatoa Trump wakati wa kampeni za uchaguzi kuhusiana na makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na Umoja wa Ulaya, baadhi ya duru za kisiasa hivi sasa zinajiuliza je, walimwengu wanapaswa kusubiri mabadiliko katika siasa za Marekani kuhusiana na makubaliano hayo ya nyuklia?

Moja ya vikao vya Iran na kundi la 5+1

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya Televisheni ya CNN kwamba, makubaliano ya nyuklia na Iran sio makubaliano ya pande mbili kati ya Iran na Marekani na kwamba, makubaliano hayo ni ya pande kadhaa na kwamba, pande zote zilizohusika katika makubaliano hayo zinapaswa kuyatekeleza.

Ushirikiano jumuishi wa Iran na Umoja wa Ulaya baada ya makubaliano ya nyuklia una malengo ambayo yanapaswa kufikiwa; ingawa kuna changamoto kadhaa katika njia ya kufikia hilo. Hapana shaka kuwa, kuongezeka ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran una mambo yanayolazimu hilo ambapo mojawapo ni kuweko uwazi wa miamala wa upande wa pili katika utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.

Ni jambo lisilo na shaka kuwa, uwazi mkabala na ahadi ni jambo ambalo litakuwa na taathira chanya katika kupatikana uhusiano kwenye mambo na masuala mengine Mashariki ya Kati. Federica Mogherini, mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amekuwa akisisitiza zaidi nukta hii katika mazungumzo yake na viongozi wa Iran na kueleza kuwa, umoja huo umeahidi kutekeleza makubaliano hayo na una azma thabiti ya kupanua ushirikiano wake na Iran katika fremu ya kudhamini maslahi ya pamoja.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

Hapana shaka kuwa, kufikia malengo na maslahi ya pamoja kunafungamana na kuweko ushirikiano wenye mlingano katika nyuga mbalimbali. Uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya nao si wenye kuondolewa katika kanuni na msingi huu. Tab'an Marekani haikubaliani na fikra hii ya pamoja na ndio maana ikitumia visingizio hivi na vile, mara kadhaa imefanya njama za kuzuia kuweko uhusiano athirifu baina ya Iran na Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, bila shaka Umoja wa Ulaya daima hauwezi kuwa mateka wa siasa na matakwa ya upande mmoja ya Marekani.