Maelfu ya raia wa Sudan Kusini wakimbilia nchini Kongo
Maelfu ya raia wa Sudan Kusini wamekimbilia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia kujiri machafuko kupita kiasi nchini humo.
Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa maelfu ya wakazi wa eneo la Equator (Ikweta) la Sudan Kusini wamekimbilia katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na kushadidi machafuko katika eneo hilo.
Mmoja wa maafisa wa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa hali ya wakazi wa eneo lililotajwa huko Sudan Kusini ni mbaya sana na kwamba hatua za haraka zinapasa kuchukuliwa ili kuwadhaminia makazi, chakula na madawa raia hao. Imeelezwa kuwa jinai na hujuma mbalimbali zinajiri kwa wingi katika eneo la magharibi mwa Sudan Kusini na hali ya mambo katika eneo hilo ni mbaya sana.
Emanuel Moro Aida mmoja wa wakimbizi wa Sudan Kusini amesema kuwa na hapa ninamnukuu,"mimi mwenyewe nimeshuhudia vitendo vya uporaji, mauaji, udhalilishaji wa kingono na nyumba za raia zikichomwa moto." Mwisho wa kunukuu. Mkimbizi huyo ameongeza kusema kuwa, kuna watu ambao wanajificha maporini na kisha huwateka nyara mabinti na kuwalazimisha kuolewa na watenda jinai sambamba na kuwapikia chakula; na iwapo mabinti hao watakataa, huuawa.
Herve Ladsous Mkuu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa pia Jumatano iliyopita alisema kuwa anatiwa wasiwasi na hali mbaya ya kibinadamu huko Sudan Kusini na kuongeza kuwa mgogoro wa kibinadamu unaoikabili nchi hiyo ni maafa na kwamba mgogoro huo unapamba moto siku baada ya siku. Ladsous ameongeza kuwa katika vita hivyo vya Sudan Kusini ambavyo vinapitisha mwaka wa tatu sasa, makumi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo wameaga dunia huku wengine karibu milioni mbili wakilazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi.
Mkuu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa amezikosoa pande hasimu huko Sudan Kusini kwa kutoheshimu makubaliano ya amani na kuzitolea wito pande hizo kuheshimu makubaliano hayo.
Afisa mwingine wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ambaye hakutaja jina lake litajwe amesema kuwa watu zaidi ya elfu 50 wamuuawa katika mapigano huko Sudan Kusini.
Hii ni katika hali ambayo mapigano yangali yanaendelea nchini humo licha ya kufikiwa makubaliano ya kusaka amani mwezi Agosti mwaka jana. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon siku kadhaa zilizopita alitaka kuheshimiwa makubaliano ya amani huko Sudan Kusini kufuatia kushadidi mapigano nchini humo. Akisisitiza kuwa pande zinazozozana nchini Sudan Kusini hazina chaguo jingine isipokuwa kuheshimu makubaliano ya amani, Ban Ki-moon amesema kuwa Sudan Kusini tayari imefikia makubaliano ya kusaka amani ambayo yalisainiwa mwezi Agosti mwaka jana na kwamba upo udharura wa kuheshimiwa masharti ya makubaliano hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa serikali ya Sudan Kusini inapasa kutekeleza majukumu yake ya kuwalinda raia wa nchi hiyo.
Wakati huo huo vitendo vya uporaji, ubakaji, njaa na ukame vingali vinaikabili nchi hiyo. Wiki iliyopita vikosi vya Sudan Kusini vililazimika kuondoka katika mji wa Wau kaskazini magharibi mwa nchi hiyo kutokana na kukabiliwa na uhaba wa silaha na chakula, ambapo imeelezwa kuwa vikosi hivyo badala ya kuwalinda raia, vimetekeleza mauaji na kuiba mali za raia wa mkoa huo. Wiki iliyopita Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka pia iliripoti habari ya kujeruhiwa raia wasiopungua 35 katika shambulio la watu wenye silaha mashariki mwa Sudan Kusini. Makao ya jumuiya hiyo pia ililengwa na shambulio hilo la watu wenye silaha na baadhi ya vitu kuibiwa. Mkurugenzi wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka huko Sudan Kusini ameashiria hasara na maafa yaliyosababishwa kwa jumuiya hiyo na kueleza kuwa eneo hilo linakabiliwa na uhaba wa vifaa vya tiba na kwamba watu wanaojeruhiwa wanahitaji kufanyiwa upasuaji na kupatiwa huduma maalumu za matibabu.
Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu ulitangaza kuwa watu zaidi ya milioni mbili na laki nane sawa na robo moja ya jamii nzima ya watu wa Sudan Kusini wanahitaji msaada wa haraka wa chakula, huku wengine elfu 40 wakikaribia kukumbwa na maafa ya kibinadamu.