Kuungana makundi mawili yenye misimamo mikali huko Mali
Makundi mawili kwa majina ya Ansaruddin na al Murabitun yameamua kuungana katika hatua mpya iliyochukuliwa na makundi yanayobeba silaha yenye makao yao huko Mali.
Muungano huo mpya ulioasisiwa baada ya kuungana makundi hayo mawili umepewa jina la "Jumuiya ya Nusratul Islam Wal Muslimin" na utakuwa chini ya uongozi wa Iyad Ag-ghali kiongozi wa kundi la Ansaruddin. Muungano huo umeundwa katika hali ambayo makundi hayo mawili yenye misimamo mikali hadi sasa kwa mara kadhaa yamehusika na mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa serikali ya Mali, kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Mataifa, pamoja na wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini humo. Kundi la al Murabitun ambalo lina mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na ambalo linaongozwa na Mukhtar Bel Mukhtar al Jazairi lilihusika katika mlipuko wa kigaidi uliotekelezwa Januari 18 katika kambi ya kijeshi katika mji wa Gao, kaskazini mwa Mali. Watu 60 waliuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika mlipuko huo.
Imeelezwa kuwa makundi ya brigedi za Massina ambayo yanaendesha harakati zake katikati ya Mali na ambayo ni makundi chipukizi kutoka mtandao wa al Qaida tawi la kaskazini mwa Afrika kwa jina la Sahara Emirat hivi karibuni yanatarajia kujiunga na muungano huo mpya wa Ansaruddin na al Murabitun. Muungano huo mpya umeasisiwa huku viongozi wa Mali wakichukua hatua za kuanza kutekeleza makubaliano ya amani ya nchi hiyo ili kuhitimisha machafuko na ukosefu wa amani nchini humo.
Hata kama imepita miaka kadhaa sasa ambapo Mali inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa na makundi yanayopigania kujitenga na yale ya uasi ya wanamgambo, lakini kuzidi kuenea makundi ya kigaidi katika eneo na kuongezeka hatari ya kuweko makundi hayo, kumetoa msukumo kwa viongozi wa Mali kutekeleza makubaliano ya amani ya nchi hiyo yaliyosainiwa mwaka 2015 kati ya viongozi wa serikali na makundi mbalimbali ya wanamgambo wa nchi hiyo.
Wakati huhuo pamoja na kuwa makubaliano hayo yameshindwa kutekelezwa kwa muda sasa, lakini siku kadhaa zilizopita viongozi wa Bamako na makundi ya wanamgambo walibainisha kuwa wanafanya kila wawezalo kuchukua hatua ya kwanza ya kutekeleza makubaliano hayo kwa kuainisha viongozi watakaosimamia uongozi wa maeneo kadhaa huko kaskazini mwa Mali. Mpango wa kutumwa watawala wa kieneo katika maeneo ya Kidal, Gao, Timbuktu, Manaka na Taoudenni umeanza kutekelezwa tangu siku ya Alhamisi tarehe Pili mwezi Machi mwaka huu. Watawala hao wanaiwakilisha serikali na makundi yenye silaha ambayo yatakuwa mamlakani kati ya miezi 18 na 24 na baada ya hapo mabaraza ya kieneo kuchukua usimamizi wa maeneo hayo. Aidha askari jeshi kutoka jeshi la serikali na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali na wale wa upinzani katika kalibu ya makubaliano ya amani ya nchi hiyo tayari yako katika maeneo ya kaskazini mwa Mali tangu tarehe 13 mwezi Februari. Hatua hiyo ya viongozi wa Mali imechukuliwa baada ya kuongezeka mashambulizi ya makundi ya kigaidi nchini humo. Hatua hiyo inaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza nguvu na uwezo wa kujipenyeza makundi ya wanamgambo ya kigaidi katika eneo. Kwa msingi huo makundi hayo yameamua kutekeleza siasa za kuungana, hata hivyo uzoefu unaonyesha kuwa hata kama yameamua kuungana ikiwa ni katika juhudi za kulinda nguvu zao, lakini yapo katika hali ya kulegalega kiasi kwamba hitilafu za kimtazamo za ndani na mashinikizo kutoka nje yanaweza kupelekea kuvunjika haraka muungano wao huo. Hasa ikizingatiwa kuwa iwapo viongozi wa Mali wataafiki kuendeleza siasa zao na kwenda sambamba na makundi ya wanamgambo yaliyosaini makubaliano ya amani ya nchi hiyo, hatua hiyo itasaidia kupunguza kiwango cha mashambulizi ya kigaidi si tu ndani ya nchi hiyo pekee, bali katika eneo zima na katika mipaka ya nchi hiyo na kuzipelekea nchi jirani kuchukua hatua za kushirikiana ili kurejesha amani na uthabiti katika eneo hilo zima.