Oct 07, 2017 00:13 UTC
  • Spika Larijani: Wamarekani wanafanya uafiriti katika suala la nyuklia

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya chuki na njama za Wamarekani dhidi ya Iran kugonga mwamba baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, lakini hadi sasa wangali wanaendeleza hatua zao za chuki na wamekuwa wakifanya uafiriti katika kadhia ya nyuklia.

Dakta Ali Larijani amesema kuwa, kusimama kidete na taifa hili kuwa na moyo wa jihadi na mapambano, ni mambo ambayo yamekuwa kinga madhubuti kwa hujuma na mashambulio ya maadui.

Makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na nchi za Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani pamoja na Ujerumani maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016.

Hata hivyo hadi hivi sasa serikali ya Marekani imekuwa ikivikanyaga wazi wazi na kwa makusudi vipengee vya makubaliano hayo huku Jamhuri yya Kiislamu ya Iran ikiwa imeyaheshimu kikamilifu. Hata ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zimekuwa zikisisitiza kwamba, hakuna nyaraka wala ushahidi unaoonyesha kwamba, Iran imekiuka makubaliano ya nyuklia.

Wajumbe walioshiriki katika mazungumzo ya nyuklia

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais Donald Trump wa Marekani ambaye amekuwa akifanya jitihada za kuvuruga makubaliano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 kwa kutumia fursa na mbinu zote, kwa mara nyingine tena amedai kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitekelezi makubaliano hayo.

Wakati huo huo, hivi karibuni mabalozi wa nchi tano za Uingereza, Ubelgiji, Denmark, Poland na Uholanzi walisema kwamba makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni makubaliano ya kimataifa na kwamba pande zote zinazohusika kwenye makubaliano hayo zinapaswa kuyaheshimu.

 

Tags