Makundi ya kitakfiri yahudumia malengo ya utawala wa Kizayuni
Duru za habari zimefichua sura mpya na pana zaidi ya ushirikiano wa utawala wa Kizayuni wa Israel na makundi ya kitakfiri na kigaidi huko Syria na kutangaza kwamba, utawala huo umeunda kundi la kigaidi kwa ajili ya kuusaidia utawala huo katika maeneo unayoyakalia kwa mabavu ya Golan.
Mtandao wa The Intercept wa Marekani umefichua kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha kundi lililopewa jina la Polisi wa Mpakani linaloundwa na magaidi wa kitakfiri huko kusini mwa Syria kwa shabaha ya kulinda mipaka ya eneo linalokaliwa kwa mabavu la Golan. Itakumbukwa kuwa katika kipindi chote cha mgogoro wa Syria, Wazayuni wamekuwa wakiwasaidia wapiganaji wa makundi ya kigaidi kama Daesh na kutibu majeruhi wao katika hospitali zilizopo kwenye ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Golan. Ripoti zinasema kuwa, utawala haramu wa Israel sasa umepanua maeneo hayo unayoyakalia kwa mabavu na kujumuisha mikoa ya Quneitra na Daraa. Vilevile Wazayuni wanashirikiana na magaidi katika kusimamia na kuendesha maeneo ya Quneitra na Daraa. Msimu wa joto wa mwaka uliopita maafisa wa Israel walianza kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wapiganaji karibu 500 wa kundi lililopewa jina la "Mashujaa wa Golan" ambao sasa wanatumika kama polisi wa mpakani wa utawala huo. Kazi kuu ya kundi hilo ni kusimamia maeneo hayo ya mpakani na kutoa ripoti kwa utawala haramu wa Israel.
Ripoti mbalimbali za hivi karibuni zimekuwa zikifichua uhusiano na ushirikiano unaozidi kuimarika kati ya makundi ya kitakfiri na utawala haramu wa Israel. Kadiri siku zinavyopita pia ndivyo uhusiano huo unavyoonekana zaidi na kuonesha kuwa, Syria inakabiliwa na makundi mengi ya kigaidi yanayosaidiwa na kuungwa mkono na Israel na waitifaki wake wa Magharibi. Baada ya kushindwa kundi la kigaidi la Daesh ambalo lilikuwa mradi wa Marekani, Saudi Arabia, Israel na washirika wao katika nchi za Iraq na Syria sasa nchi hizo hizo zimeamua kutumia mbinu nyingine za kuyafadhili na kusimamia makundi ya kitakfiri na kigaidi kwa ajili ya kuendelea kusababisha fitina, ghasia na migawanyiko huko Syria hususan katika maeneo yanayopakana na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Ukweli ni kwamba, harakati hizo za kijeshi na kigaidi za Israel dhidi ya Syria zinaenda sambamba na fitina zinazofanywa na utawala huo na washirika wake kwa ajili ya kuishughulisha Syria na migogoro ya ndani. Gazeti la al Quds al Arabi linalochapishwa London nchini Uingereza liliripoti siku chache zilizopita kwamba: Israel imekuwa ikifaidika na matukio ya kigaidi yanayotokea duniani likiwemo shambulizi la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani. Mwandishi wa ripoti hiyo, Muhammad Abbas amesisitiza kuwa utawala ghasibu wa Israel unayatambua mashambulizi ya kigadi kuwa ni fursa nzuri kwa ajili ya kufikia malengo yake.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, makundi ya kigaidi yanayofanya harakati katika nchi za Mashariki ya Kati kama Syria na Iraq hayawezi kuendelea kuwepo bila ya misaada ya fedha na silaha ya nchi za kigeni na utawala haramu wa Israel. Moja ya malengo ya kuundwa na kuimarishwa makundi hayo ya kigaidi ni kuzitumbukiza nchi za Kiislamu na eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla katika migogoro ya ndani na kuzishughulisha kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na hatimaye kuzidhoofisha nchi za eneo hilo hususan zile zilizoko mstari wa mbele wa muqawama na mapambano mkabala wa Israel. Lengo jingine ni kuwasahaulisha Waislamu kadhia yao nambari moja yaani Quds na kibla chao cha kwanza kinachokaliwa kwa mabavu na Israel. Hata hivyo njama hizo zinazoungwa mkono na baadhi ya nchi zinazojiita za Kiislamu kama Saudi Arabia zimejulikana waziwazi na kuna ulazima kwa Umma hususan nchi zilizoko mstari wa mbele katika kambi ya mapambano kuwa macho zaidi na zaidi.