Marekani, nchi ambayo daima iko vitani
Sera za kijeshi na za kupenda vita za Marekani zinakosolewa kote duniani na hivi sasa hata wakuu wa nchi hiyo wameanza kukosoa sera hizo.
Jimmy Carter, rais wa 39 wa Marekani kutoka mwaka 1977 hadi 1981, katika mahojiano na jarida la Time amesema tokea kuanzishwa Umoja wa Mataifa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia hadi sasa, Marekani daima imekuwa vitani.
Rais huyo wa zamani wa Marekani ambaye aliwahi kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel, amesema tangu kumalizika Vita Vikuu Vya Pili vya Dunia Marekani imeanzisha vita katika nchi 30 duniani.
Matamshi ya rais wa zamani wa Marekani ni dalili ya wazi kuwa nchi hiyo haiwezi kutekeleza mipango yake ya kiuchumi na kisiasa pasina kuwepo vita.
Kwa hakika, Marekani katika muundo wake wa sasa iliibuka katika nusu ya pili ya karne ya 18 baada ya kupigana vita vya uhuru na Ufalme wa Uingereza. Tokea wakati huo nchi hiyo kimsingi imekuwa vitani. Marekani ilipigana vita na Uingereza mwaka 1812, kisha ikaingia vitani na Mexico mwaka 1846 na vita na Uhispania mwaka 1898. Kisha iliingia katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia mwaka 1917 na baada ya hapo ikaingia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilivyoanza mwaka 1941. Baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Marekani iliendeleza sera zake za kichokozi na vita kwa kisingizio cha kutetea kile inachodai kuwa ni uhuru duniani. Hapa tunaweza kutaja baadhi ya vita ambavyo Marekani imejihusisha navyo tokea wakati huo ambavyo ni, Vita vya Korea mwaka 1950, Vita vya Vietnam kuanzia nusu ya pili ya muongo wa 1960, hujuma dhidi ya nchi ya Kisiwa cha Grenada mwaka 1983, kukalia kijeshi Panama mwaka 1989, hujuma dhidi ya Iraq mwaka 1991, hujuma dhidi ya Afghanistan mwaka 2001, hujuma nyingine dhidi ya Iraq mwaka 2003 na hujuma dhidi ya Libya mwaka 2011. Hiyo ni mifano muhimu ya vita ambavyo Marekani imehusika navyo katika kipindi cha miaka 70 iliyopita. Mbali na hayo, katika kipindi hicho, Marekani imejihusisha na oparesheni kadhaa za kijeshi kote duniani na pia kuongoza au kuchochea mapinduzi ya kijeshi.
Mbali na hayo Marekani pia ilichochoea na kuhusika na vita baridi na Shirikisho la Zamani la Sovieti. Hivi sasa Marekani aidha inahusika na oparesheni kadhaa za kijeshi kote duniani katika kile inachodai kuwa ni vita dhidi ya ugaidi lakini uhalisia wa mambo ni uingiliaji masuala ya ndani ya nchi zingine.
Hataka kama hakuna takwimu kamili zilizopatikana kuhusu idadi ya watu waliouawa kaitka vita ambavyo Marekani imeshusika navyo kote duniani, lakini tunaweza kusema kuwa katika kipindi cha miaka 240 iliyopita hadi sasa, mamillioni ya watu wameuawa kutokana na sera za kivita za Marekani.
Hapa tunaweza kuashiria matukio mawili ya kudondoshwa mabomu ya atomiki katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan katika muda wa siku mbili ambapo watu 220,000 walipoteza maisha. Nchi nyingi duniani zinaendelea kushuhudia hasara kubwa zinazotokana na vita vilivyosababishwa na Marekani duniani. Nchi zinazopata hasara kubwa kutokana na vita hivyo ni nchi zinazostawi au nchi masikini duniani.
Utafiti umebaini kuwa uchumi wa Marekani hauwezi kustawi ila kwa nchi hiyo kueneza vita katika maeneo mbali mbali duniani. Kwa msingi huo kwa serikali ya Marekani, na vile vile kwa Wamarekani wengi, vita ni jambo lisiloweza kuepukika. Kwa muundo wake wa sasa , ni vigumu Marekani isitishe sera zake za kichokozi na kivita.