Saudi Arabia kutayarisha 'mkataba wa ushirikiano wa muda mrefu' na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101234-saudi_arabia_kutayarisha_'mkataba_wa_ushirikiano_wa_muda_mrefu'_na_iran
Akiwa njiani kurejea kutoka ziara ya siku mbili nchini Saudi Arabia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema wakuu wa ufalme huo wameagiza kuanzishwa kwa hatua za awali za kubuni "makubaliano ya muda mrefu ya ushirikiano" na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 19, 2023 03:40 UTC
  • Saudi Arabia kutayarisha 'mkataba wa ushirikiano wa muda mrefu' na Iran

Akiwa njiani kurejea kutoka ziara ya siku mbili nchini Saudi Arabia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema wakuu wa ufalme huo wameagiza kuanzishwa kwa hatua za awali za kubuni "makubaliano ya muda mrefu ya ushirikiano" na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa waliokuwa ndani ya ndege iliyokuwa ikimrudisha Iran kutoka Saudia kwamba, Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman amemuamuru Waziri wa Mambo ya Nje wa ufalme huo Faisal bin Farhan kuwa hatua za awali zichukuliwe katika kutayarisha hati ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi mbili.

Amir-Abdollahian ameongeza kuwa baada ya kukamilika hati hiyo itatiwa saini na maafisa wa ngazi za juu wa Iran na Saudi Arabia.

Ziara ya Amir-Abdollahian, ya kwanza kufanywa na waziri wa mambo ya nje wa Iran katika ufalme huo katika zaidi ya muongo mmoja, inaashiria hatua kubwa katika uhusiano wa nchi hizi mbili jirani.

Uhusiano huo ulikatishwa na Saudi Arabia Januari 2016, baada ya waandamanaji wa Iran, waliokasirishwa na kunyongwa kwa kiongozi mashuhuri wa Kishia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr na serikali ya Saudi Arabia, kuvamia ubalozi wa Saudia mjini Tehran.

Mnamo Machi mwaka huu, Iran na Saudi Arabia zilifikia makubaliano ya maridhiano baada ya siku kadhaa za mazungumzo makali yaliyoandaliwa na China.

Akifafanua mazungumzo yake wakati wa safari hiyo na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, ambaye kimsingi ndiye mtawala wa nchi hiyo, waziri wa mambo ya nje amesema mkutano wake na Mohammad bin Salman ulidumu kwa muda wa "dakika 90 ambapo asilimia 70 ya mazungumzo yaliangazia maswala ya pande mbili."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Saudi Arabia imejitahidi katika ziara hiyo kusisitiza kuwa imechukua "mtazamo mpya" ikilinganishwa na siku za nyuma.

Viongozi wa Saudia, wamebainisha, wamejaribu kuonyesha utayari wao wa kufungua "ukurasa mpya katika mahusiano ya nchi hizi mbili."

Wakati huo huo Amir-Abdollahian ametangaza kuwa Iran imemwalika mwana mfalme wa Saudia kufanya ziara katika Jamhuri ya Kiislamu.

Ameendelea kusema kuwa, Kiongozi huyo wa Saudia amekubali mwaliko huo, akisema atapanga mipango muhimu ya kutembelea Tehran "wakati unaofaa."