Jun 28, 2016 14:06 UTC
  • Maelfu waendeleza mgomo mbele ya nyumba ya Ayatullah Qasim, Manama

Maelfu ya Wabahrain wameendelea kufanya mgomo wa kuketi chini mbele ya nyumba ya Kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini huyo, Ayatullah Isa Qasim kwa siku ya nane mfululizo huku wakipiga nara zinazopinga utawala wa kifalme wa nchi hiyo.

Watu hao pia wameitaka serikali ya Manama kumrejeshea uraia Ayatullah Qasim ambao alivuliwa siku chache zilizopita na kutoa wito wa kukomeshwa ushawishi wa kizazi cha Aal Khalifa nchini humo na vilevile ubaguzi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia waliowengi nchini Bahrain.

Ripoti zinasema serikali ya Bahrain imeendelea kulizingira eneo la Deraz na kuzuia mamia ya Waislamu kuingia katika eneo hilo kwa kisingizio kwamba si wakazi wa eneo hilo. Hata hivyo maelfu miongoni mwao wamefanikiwa kupenya na kuingia katika eneo hilo mjini Manama na kujiunga na mgomo wa kuketi chini licha ya hatua kali za kiulinzi.

Tarehe 20 mwezi huu utawala wa kizazi cha Aal Khalifa nchini Bahrain ulimvua uraia mwanazuoni mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu nchini humo Ayatullah Isa Ahmad Qasim.

Siku mbili baadaye ilifichuka kwamba. Mfalme wa Saudia Salman bin Abdulaziz ndiye aliyetoa amri kwa utawala wa Bahrain kufuta uraia wa Sheikh Isa Qasim.

Mfalme Salman alitoa amri hiyo kupitia barua aliyomwandikia Hamad bin Isa Al Khalifa, mtawala wa Bahrain.

Tags