OIC yalaani ongezeko la hujuma dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani vikali vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Katika taarifa, OIC imelaani ukiukaji unaoendelea kufanywa dhidi ya Msikiti unaoheshimika wa Al-Aqsa mjini al Quds na kusisitiza udharura wa jamii kimataifa kuingilia na kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unavamia mara kwa mara eneo hilo takatifu.
Taarifa ya OIC imesisitiza kwamba, Msikiti wa al-Aqsa na jengo lake kubwa ni mahali pa ibada kwa ajili ya Waislamu pekee.
Hivi karibuni, sambamba na maadhimisho ya sikukuu za Kiyahudi, makumi ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada waliuvamia msikiti mtakatifu wa al-Aqsa na kufanya vitendo vya kichochezi.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.
Tangu serikali ya Waziri Mkuu Benjamini Netanyahu ishike tena hatamu za uongozi huko Israel, hujuma na uvamizi wa mara kwa mara wa walowezi wa Kizayuni umechukua mkondo mpana zaidi.
Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.