Kurejea mitaani waandamanaji kumpinga Netanyahu
(last modified Mon, 23 Oct 2023 04:34:59 GMT )
Oct 23, 2023 04:34 UTC
  • Kurejea mitaani waandamanaji kumpinga Netanyahu

Wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel, kwa mara nyingine wamemiminika mitaani kushinikiza kujiuzulu waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.

Miezi 10 imepita  tangu iundwe serikali yenye misimamo mikali ya Kizayuni huko Israel chini ya uwaziri mkuu wa nduli, Benjamin Netanyahu. Katika kipindi hiki cha miezi 10, Netanyahu ametumia njia zote za kikatili kuhakikkisha anabakia madarakani na anakabiliana na mashinikizo makubwa ya wanaomtaka ajiuzulu na halafuu apandishwe kizimbani kwa ufisadi wake yeye, na familia yake. Wakazi wa utawala wa Kizayuni wamekuwa wakifanya maandamano makubwa ya mamia ya maelfu ya watu ambayo yameweka rekodi katika maandamano ndani ya utawala huo pandikizi, wakishinikiza kujiuzulu Netanyahu. Lakini muda wote huu, waziri mkuu huyo wa Israel amekuwa akitumia hila mbalimbali za kikatili na kishetani kukandamiza waandamanaji au kuwashambulia kinyama Wapalestina, au kufanya mashambulio nje ya ardhi za Palestina, ili kupunguza mashinikizo dhidi yake. 

Sababu kuu iliyoshadidisha mashinikizo ya kutaka Netanyahu ajiuzulu, ni mpango wake wa kufanyia marekebisho mfumo wa mahakama wa utawala wa Kiayuni ili kuivunja nguvu idara ya mahakama na kuizidishia nguvu serikali. Wapinzani wa Netanyahu wanaamini kuwa mpango huo ni sehemu ya njama za waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni za kutawala kidikteta na kuidhibiti mihimili mengine ya dola ili awe salama mbele ya shutuma nzito za ufisadi zinazomkabili. 

 

Maandamano ya wakazi wa utawala wa Kizayauni yalisimama kidogo baada ya kutokea operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa, siku ya Jumamosi ya tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba, ambapo wanamapambano wa Palestina hasa wale wa Kataib za al Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS walitoa pigo kubwa la kijeshi na kijasusi kwa utawala wa Kizayuni. Lakini maandamano hayo yalisimama kwa muda wa wiki mbili tu, baada ya hapo maelfu ya wakazi wa Tel Aviv, Jumamosi ya juzi walimiminika tena mitaani kushinikiza kujiuzulu Benjamin Netanyahu.

Hoja kubwa inayotumiwa hivi sasa na waandamaji wanaoshinikiza waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni ajiuzulu, ni kutojali kwake hali ya mateka wa Israel walioko mikononi mwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Netanyahu anaendelea kufanya mashambulio ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza na hafanyi juhudi zozote za kuwakomboa mateka wa Israel. Bali hata zimeenea habari kuwa, Netanyahu hazimshughulishi roho za mateka hao wa Israel na huenda akaanzisha vita vya nchi kavu huko Ghaza kwa shabahha ya kuwaua mateka hao.

Netanyahu anaendelea kufanya jinai Ukanda wa Ghaza, lakini jinai hizo haziwezi kumuokoa na kitanzi cha kuburuzwa mahakamani kujibu mashitaka mazito ya ufisadi

 

Mbali na kurejea watu mitaani kumpinga Netanyahu, uchunguzi wa maoni nao unaonesha kukwa wakazi wengi wa utawala wa Kizayuni wanataka Benjamin Netanyahu ajiuzulu. Gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post limeandika kuwa, matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonesha kuwa, wakazi wengi wa utawala wa Kizayuni, yaani asilimia 56 ya wakazi hao wanataka Netanyahu ajiuzulu mara vitakaposimamishwa vita vya Ghaza. Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, ni asilimia 28 tu ya wakazi wa utawala wa Kizayuni wanaomuunga mkono Netanyahu katika vita anavyoendelea navyo hivi sasa huko Ghaza. Ripoti ya gazeti hilo la Kizayuni imefichua pia kwamba, kati ya kila Waisraeli watano, wanne wanaamini kuwa Netanyahu mwenyewe na serikali yake ndio wanaopaswa kubeba lawama za kutokea operesheni ya  #Kimbunga_cha_al-Aqsa na kupata kipigo kikubwa utawala wa Kizayuni. 

Maandamano ya wakazi wa utawala wa Kizayuni na matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni ni uthibitisho kuwa mashambulio makubwa na ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza na kuuliwa kwa umati watoto, wanawake na wananchi wa kawaida kwenye eneo hilo, si tu hakujamsaidia Netanyahu na serikali yake mbele ya hatari ya kusambaratika, lakini pia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali hiyo kwenye vita vya Ghaza, zimekuwa ni sababu nyingine ya mashinikizo ya wakazi wa utawala wa Kizayuni ya kumtaka Netanyahu ajiuzulu. Waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni alikuwa na ndoto kwamba, vita vya pande zote dhidi ya Wapalestina na kuua kwa umati wanawake na watoto wadogo kutaweza kubadilisha hisia za watu ndani ya utawala wa Kizayuni na kumuokoa na kesi nzito za ufisadi zinazomkabili yeye na familia yake lakini ndoto hizo zimeendelea kubakia kuwa za alinacha. Iwapo Netanyahu hatofanya juhudi za kuwaokoa mateka wa Israel wanaokadiriwa kufikia 210 walioko mikononi mwa HAMAS, basi hakutokuwa na kitu chochote cha kuzuia kuporomoka yeye na serikali yake.