Kuongezeka kukosolewa uungaji mkono wa Magharibi kwa utawala wa Kizayuni
Kuendelea jinai , mauaji ya kimbari na kutokomezwa kizazi cha wananchi wa Gaza na utawala wa Kizayuni ambazo zimesababisha maelfu ya Wapalestina kuuawa shahidi na kujeruhiwa, kumepelekea kushtadi kukosolewa siasa za upendeleo za serikali za Magharibi kwa Israel.
Wawakilishi wa kisiasa na wafanyakazi wa serikali ya Marekani wapatao zaidi 400 wamemtumia barua Rais Joe Biden wa nchi hiyo wakipinga uungaji mkono wake kwa utawala wa kibaguzi wa Israeli katika vita vya Gaza. Maafisa hao wanawakilisha takriban mashirika 40 ya serikali, na barua yao ni sehemu ya upinzani unaoongezeka dhidi ya siasa za seriakli ya Biden kuhusiana na vita vinavyoendelea huko Gaza. Waandishi wa barua hiyo wamemtaka Biden asitishe mapigano mara moja huko Gaza na kuanda uwanja wa kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.
Barua hiyo ni moja tu ya barua kadhaa za malalamiko ambazo zimetumwa kwa viongozi wa ngazi za juu wa Marekani kuhusiana na suala hilo. Katika siku chache zilizopita, vyombo vya habari vimeripoti kutumwa hati tatu za malalamiko ya ndani kwa Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, ambazo zimesainiwa na makumi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo. Siku chache zilizopita, zaidi ya wafanyakazi 1,000 wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani walikosoa sera za Washington katika barua ya wazi.
Barani Ulaya hali ni hiyo hiyo na maandamano ya kupinga uungaji mkono wa viongozi wa nchi hizo kwa utawala wa Kizayuni yameongezeka. Kuhusiana na suala hilo, katika hatua ambayo inaweza kuchukuliwa kuwa ni aina ya uasi wa kidiplomasia, kundi la mabalozi 10 wa Ufaransa katika nchi za Kiislamu za Asia Magharibi wamepinga siasa za upendeleo za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa utawala wa Kizayuni kwa kuandika barua. Barua hiyo inasema: "Watu wetu wanahisi kwamba tunajisaliti wenyewe. Wanaamini kwamba siasa zetu juu ya haki za binadamu zinapingana na vitendo vyetu." Katika barua yao, mabalozi hao wamekosoa kile walichokiita kujitenga Macron na msimamo wa jadi kuhusiana na suala la mzozo wa Israel na Palestina na kutozingatia serikali yake siasa za udiplomasia katika ulimwengu wa Kiarabu suala ambalo halijawahi kutokea tena huko nyuma
Baada ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, rais wa Ufaransa alitangaza wazi uungaji mkono wake kwa Israel na kutaka kuundwa muungano wa kimataifa wa kupambana na Daesh na Hamas. Macron bila ya kutaja jinai zozote za kivita za utawala huo alikariri madai ya eti haki ya Israel kujilinda.
Nukta muhimu ni kwamba, kuongezeka hasira na chuki za kimataifa dhidi ya serikali za Magharibi kutokana na uungaji mkono wao usio na mipaka kwa jinai za Israel huko Gaza, na barua za ukosolewaji viongozi wa Ulaya na Marekani, kinyume na taratibu za serikali za huko nyuma kunaonyesha kuenea mbinu hii muhimu ya malalamiko hata kwenye vyombo vya serikali hizo. Serikali ya Biden imepokea maonyo ya wanadiplomasia wake katika nchi za Kiarabu, ambayo yanakemea uungaji mkono mkubwa wa Marekani kwa Israel katika vita vya uharibifu na kijinai vya utawala wa Kizayuni huko Gaza na kutahadharisha kuwa unaweza kupelekea kupungua satwa ya nchi hiyo miongoni mwa kizazi kizima katika nchi za Waarabu.
Masuala hayo yanaonyesha kuwa tofauti na siku za nyuma na hata mwanzoni mwa vita vya Ghaza, ambapo utawala wa Kizayuni ulijaribu kuhadaa fikra na hisia za walimwengu kwa kuchapisha habari na kuonyesha video za uwongo ili kuhalalisha vitendo vyake vya kijinai dhidi ya watu wa Gaza, hivi sasa walimwengu na viongozi wa nchi mbalimbali wamefahamu undani wa jinai za utawala huo dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza kupitia uchapishwaji wa habari, ripoti na picha za moja kwa moja kutoka ukanda huo, jambo ambalo limeamsha hisia za kimataifa na kuipelekea jamii ya kimataifa kutaka kulazimishwa Tel Aviv isitishe mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Katika kujibu jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina, Rais Lula da Silva wa Brazil amesema: Mashambulizi ya Israel dhidi ya wanawake na watoto huko Ghaza ni jinai. Israel inataka kuteka Ukanda wa Gaza na kuwalazimisha Wapalestina kuwacha ardhi zao. Hii sio sawa wala haki.