UNRWA: Gaza imekuwa 'mojawapo ya maeneo hatari zaidi' duniani
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) leo Jumatano limesema kuwa Ukanda wa Gaza sasa ni "mojawapo ya maeneo hatari zaidi" duniani, huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendeleza mashambulizi na mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo la Palestina linalozingirwa.
UNRWA imesema katika taarifa yake kupitia ukurasa wa X kwamba: "Ukanda mzima wa Gaza umekuwa mojawapo ya maeneo hatari zaidi duniani."
UNRWA pia imesema "hakuna tena mahali pa kupata hifadhi" huko Gaza, na kuongeza kuwa makazi ya UNRWA yenyewe hivi sasa "yamefurika" na watu waliokimbia makazi yao.
Siku ya Jumatatu, UNRWA ilisema zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa Gaza kwa sasa wamekimbia makazi yao yaani karibu watu milioni 1.9 kati ya jumla ya watu milioni 2.3 wanaoishi eneo hilo la pwani na kuongeza kwamba karibu wakimbizi wa ndani milioni 1.2 wamepewa hifadhi katika vituo 156 vya UNRWA.
Israel ilianza tena vita vya maangamizi ya umati dhidi ya ardhi ya Palestina siku ya Ijumaa baada ya kumalizika usitishaji vita wa wiki moja ya misaada ya kibinadamu na kundi la Palestina Hamas.
Takriban Wapalestina 16,248 wameuawa shahidi, wengi wakiwa ni wanawake na watoto na wengine zaidi ya 43,616 wamjeruhiwa katika mashambulizi ya anga na nchi kavu kwenye eneo hilo tangu Oktoba 7.