Hamas: Hakuna kubadilishana mateka bila kusimamishwa vita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105896-hamas_hakuna_kubadilishana_mateka_bila_kusimamishwa_vita_gaza
Mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema iwapo hujuma ya utawala wa Kizayuni huko Gaza haitasimamishwa, hakuna mazungumzo yoyote yatakayofanyika kuhusu kubadilishana mateka wa Kizayuni na Wapalestina.
(last modified 2024-05-29T07:24:47+00:00 )
Dec 12, 2023 03:54 UTC
  • Hamas: Hakuna kubadilishana mateka bila kusimamishwa vita Gaza

Mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema iwapo hujuma ya utawala wa Kizayuni huko Gaza haitasimamishwa, hakuna mazungumzo yoyote yatakayofanyika kuhusu kubadilishana mateka wa Kizayuni na Wapalestina.

Jumatatu jioni, baadhi ya vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni, ikiwemo Kanali 12 ya utawala huo, vilidai kuwa kumefikiwa maafikiano mapya kuhusu kubadilishana mateka.

Kwa mujibu wa  Al-Jazeera, Osama Hamdan, mwanachama mkuu wa harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, amesema leo kwamba lengo la  Israel la kutoa madai hayo ni kukabiliana na mashinikizo ya ndani kuhusiana na suala hilo.

Wanamapambano wa Harakati ya Hamas

Hapo awali, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Jihad Islami ya Palestina pia alikanusha ripoti za vyombo vya habari vya Kizayuni kuhusiana na mazungumzo ya kubadilishana mateka na kusisitiza kwamba mazungumzo ya aina yoyote kuhusu mateka hao yatafanyika baada ya usitishaji vita.

Hii ni katika hali ambayo askari wa Kizayuni jana walivamia nyumba za wafungwa walioachiwa huru hivi karibuni katika eneo la Yabud, lililoko kusini magharibi mwa Jenin na moja ya maeneo ya mji wa Al-Bireh katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Palestina huko Gaza ametangaza kuwa, Wapalestina zaidi ya 18,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 49,000 kujeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la Israel katika ukanda huo tangu tarehe 7 Oktoba.