Wafanyakazi wa utawala wa Biden waandamana kupinga vita Gaza
Wafanyakazi wa utawala wa Rais Biden wa Marekani wameandamana mbele ya Ikulu ya White House, wakitoa wito wa kusitishwa vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Makumi ya wafanyakazi wa serikali ya Marekani, wakiwemo walioteuliwa kisiasa, walikusanyika mbele ya Ikulu ya White Jumatano jioni kushiriki maandamano hayo ya amani. Wengi wa washiriki walivaa miwani ya jua na vinyago ili kuficha utambulisho wao.
Waandamanaji walibeba bango lililosomeka "Rais Biden, wafanyikazi wako wanataka kusitishwa mapigano". Walitaja vita vya Israel dhidi ya Gaza kuwa visivyokubalika.
Huku wafanyikazi wakiweka maua ya waridi kando ya mishumaa kuwakumbuka Wapalestina waliouawa vitani Gaza, walisoma majina ya Wapalestina waliouawa tangu Desemba 1 kufuatia kumalizika kwa usitishaji vita wa siku moja.
Josh Paul, afisa wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ambaye alijiuzulu kazi yake mwezi Oktoba kwa kupinga msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israel, alitoa hotuba ya ufunguzi.
Alisema kuwa mapatano ya usitishaji vita wa muda yaliyomalizika karibu wiki mbili zilizopita hayakutosha kamwe kwani kuanza tena kwa mauaji, kufurushwa na kushambuliwa raia wa Palestina huko Gaza kumetisha kila mtu.
Paul, ambaye alikuwa mkurugenzi wa bunge na masuala ya umma wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Masuala ya Kisiasa na Kijeshi kwa zaidi ya miaka 11, alijiuzulu mwezi Oktoba akipinga hatua ya Marekani kuipa Israel silaha.
Biden amekabiliwa na wito unaoongezeka wa kuunga mkono usitishaji. Mwezi uliopita, zaidi ya wafanyakazi 800 wa serikali ya kitaifa na majimbo Marekani walitia saini barua, wakitaka msaada wa haraka wa Biden kwa usitishaji wa mapigano na usimamishaji wa haraka wa ghasia huko Gaza.