Kuongezeka mashinikizo ya familia za mateka wa Israel dhidi ya Netanyahu
Kutokana na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, kushindwa kuwakomboa mateka wa Kizayuni kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Hamas, mashinikizo ya ndani dhidi ya waziri mkuu huyo wa utawala ghasibu yameongezeka.
Baada ya Netanyahu kuanzisha vita dhidi ya Ukanda wa Gaza, alitangaza malengo mawili makuu ya kijeshi katika vita hivyo, ambayo ni kuiangamiza Hamas na kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni waliotekwa na wapiganaji hao wa ukombozi wa taifa la Palestina. Mwezi wa tatu wa vita dhidi ya Gaza unamalizika, lakini ni wafungwa 70 pekee wa Kizayuni ndio wameachiwa huru tena kwa masharti ya Hamas na sio kupitia operesheni ya kijeshi ya baraza la mawaziri la Netanyahu. Zaidi ya wafungwa 140 wa Kizayuni bado wako mikononi mwa wapiganaji wa Hamas, na baraza la mawaziri la Netanyahu bado halijafanikiwa kuwaokoa. Wakati huo huo, habari za kuuawa baadhi ya mateka hao kupitia mashambulio ya kinyama yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni wenyewe katika Ukanda wa Gaza zilitangazwa hivi karibuni.
Suala hili pia limepelekea familia za mateka kuwa na wasiwasi maradufu kuhusu usalama wao. Kuhusiana na hilo, kufuatia ukosoaji mkubwa unaofanyika dhidi ya Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziri kuhusiana na uendeshaji mbaya wa vita na Hamas, vyombo vya habari viliripoti Jumatatu jioni kwamba alizomewa vikali na familia za mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na Hamas alipokuwa akizungumza katika bunge la utawala haramu wa Israel.
Nukta muhimu ni kwamba imani ya familia za mateka kwa Netanyahu imepungua sana ambapo familia hizo haziamini tena ahadi zake. Netanyahu amedai kuwa atawarudisha nyumbani mateka wote, lakini kwamba itachukua muda zaidi kutimiza lengo hilo. Matamshi hayo ya Netanyahu yamekabiliwa na majibu makali ya familia za mateka ambazo haziamini kwamba anaweza kuwaokoa mateka kupitia vita. Wachambuzi na weledi wengi wa Kizayuni pia wanaamini kuwa, kuendeleza vita kwa lengo la kuwaokoa mateka ni lengo lisilotekelezeka na lisiloweza kufikiwa.
Hii si mara ya kwanza kwa Netanyahu kupingwa na kulalamikiwa na familia za mateka. Katika wiki zilizopita, familia hizo pamoja na idadi kubwa ya walowezi wanaoishi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, waliandamana kupinga kuendelea vita vya Gaza na kulitaka baraza la mawaziri la vita la Israel lisitishe vita na kufanya mazungumzo na Hamas badala ya kuendesha vita ambavyo halitashinda. Kwa upande mwingine, Netanyahu ambaye anafahamu vizuri hasira ya familia za mateka wa Kizayuni kuhusiana na suala hilo, siku chache zilizopita alikutana na baadhi tu ya familia hizo, jambo ambalo limezidisha maandamano na ukosoaji dhidi yake katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Gazeti la Kiyahudi la Haaretz limemnukuu mmoja wa ndugu wa mateka hao akisema: "Tutakuwa tukikusanyika mbele ya Wizara ya Vita siku zote za wiki. Ninajua kwamba wanatumia kila njia ili kutukwepa kwa sababu wanahisi kuwa ni wahalifu."
Mbali na masuala tuliyoyataja, mauaji ya mateka watatu wa Kizayuni katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza pia yamezidisha mashinikizo ya ndani dhidi ya Netanyahu. Gazeti la The New York Times limeandika kuwa, kuuawa mateka wa Kizayuni huko Gaza kumeongeza shaka na wasiwasi kwa walowezi wa Kizayuni iwapo kweli Natanyahu anaweza kushinda vita dhidi ya Hamas.