HAMAS: Muqawama utaipa Israel funzo lisilosahaulika kwa ukatili inaowafanyia Wapalestina
(last modified Tue, 02 Jan 2024 14:20:41 GMT )
Jan 02, 2024 14:20 UTC
  • HAMAS: Muqawama utaipa Israel funzo lisilosahaulika kwa ukatili inaowafanyia Wapalestina

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani kifo cha mateka mwengine wa Kipalestina aliyeuliwa kwenye kituo cha mahabusu cha utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuahidi kuupa utawala huo funzo lisilosahaulika kutokana na ukatili wake unaoendelea kuwafanyia Wapalestina.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema, "maghasibu wa Kizayuni wamefanya mauaji ya saba ya wafungwa wetu kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kwa kumuua Abdul Rahman al-Bahsh katika Gereza la Megiddo".

Taarifa hiyo imeendelea kueleza: "tunalaani kuendelea kwa mauaji hayo huku kukiwa na ukimya wa mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na makundi ya kutetea wafungwa wa vita".

Hamas imebainisha kuwa vifo vya mateka wa Kipalestina hatimaye vitaudhuru utawala ghasibu wa Tel Aviv.

Katika taarifa tofauti, harakati hiyo ya Muqawama wa Palestina imeitaka Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) na mashirika ya haki za binadamu kubeba majukumu yao kuhusiana na mateka Wapalestina.

Shahidi Abdul Rahman al-Bahsh

Tume inayoshughulikia Mateka Wapalestina na Walioachiwa huru ilitangaza katika taarifa yake Jumatatu jioni kwamba Bahsh, mwenye umri wa miaka 23, ambaye alikuwa kifungoni tangu Mei 31, 2022, na baadaye kuhukumiwa kifungo kwa kilichoitwa "makosa ya usalama", amefia katika Gereza la Megiddo.

Tume hiyo imesema Jeshi la Magereza la Israel (IPS) linaendelea bila kujali kuwaua wafungwa zaidi wa Kipalestina katika vituo vyake vya mahabusu, na kuwaweka katika mazingira ya mateso na unyanyasaji wa kimpangilio.

Bahsh, ambaye alikuwa mwanachama wa harakati wa Muqawama ya Fat-h, amekuwa mateka wa saba wa Kipalestina kufia kwenye mahabusu za utawala wa Kizayuni wa Israel tangu Oktoba 7 wakati makundi ya muqawama yenye m makao yao Gaza yalipotekeleza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa.../

 

Tags