Sisitizo la chama cha Likud la kuuliwa Wapalestina zaidi
(last modified Tue, 12 Jul 2016 07:29:12 GMT )
Jul 12, 2016 07:29 UTC
  • Sisitizo la chama cha Likud la kuuliwa Wapalestina zaidi

Licha ya jamii ya kimataifa kulalamikia vikali mashinikizo ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, kundi moja la wabunge wa utawala huo katili limekutana na kuhimiza kuongezwa mashinikizo ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi dhidi ya Wapalestina.

Wabunge wa chama chenye misimamo ya kufutu mipaka cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kimetoa tamko na kutangaza uungaji mkono wao kwa ukandamizaji na unyanyasaji unaofanywa na serikali ya Israel dhidi ya Wapalestina na kuhimiza mauaji zaidi yafanyike dhidi ya Wapalestina hao. Wabunge hao Wazayuni wamesema, Baraza la Mawaziri la Israel linapaswa liendelee kuwaua Wapalestina hususan viongozi wa Intifadha, liharibu nyumba za wanamapambano wa Palestina na lipanue ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye ardhi wanazoporwa Wapalestina ili kwa njia hiyo, serikali hiyo iweze kuzima malalamiko na Intifadha ya Wapalestina. Mwito huo usio na chembe ya utu uliotolewa na wabunge makatili wa utawala wa Kizayuni umekuja huku bunge la utawala huo dhalimu, likipasisha muswada wa kujengwa vitongoji zaidi vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina hususan karibu na mji wa al Khalil, kama njia ya kukabiliana na Intifadha ya Wapalestina. Muda mfupi baada ya kupasishwa muswada huo, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alilipongeza bunge hilo na kuzitaka taasisi zote za utawala wa Kizayuni zipuuze malalamiko ya walimwengu na ziendeleze ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Uungaji mkono wa bunge la Israel kwa mpango wa kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa madai ya kukabiliana na Intifadha ya Quds ya wananchi wa Palestina iliyoanza mwezi Oktoba mwaka jana umekuja katika hali ambayo waungaji mkono wa utawala huo pandikizi kama vile Umoja wa Ulaya na Marekani, katika siku za hivi karibuni walisema kuwa, siasa hizo ghalati za Israel ni kizuizi katika juhudi za kuleta amani Mashariki ya Kati. Njama za taasisi na viongozi wa utawala wa Kizayuni za kuongeza mashinikizo ya kila upande dhidi ya Wapalestina zinafanyika katika hali ambayo utawala huo katili umeshindwa kukabiliana na Intifadha ya Wapalestina licha kufanya ukandamizaji na mauaji makubwa dhidi ya Wapalestina hao kiasi kwamba hadi hivi sasa Wapalestina 225 wameshauawa shahidi tangu mwezi Oktoba mwaka jana na mamia ya wengine kujeruhiwa. Kwa kweli daima Wapalestina wamethibitisha kuwa, si tu hawababaishwi na vitisho vya utawala huo wa ubaguzi wa kizazi na jinai zake, lakini pia vitendo vya kujitanua vya Wazayuni haviwazuii Wapalestina hao kuendeleza harakati zao za kupigania ukombozi wa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni uliopachikwa jina la Israel. Si hayo tu, lakini pia, uzoefu unaonesha kuwa, kila utawala wa Kizayuni unaposhadidisha mashinikizo dhidi ya Wapalestina, ndipo huwa unaandaa mazingira ya kuanza Intifadha mpya na pana zaidi ya kupambana na ukatili wa utawala huo pandikizi.