Makumi ya magaidi wakufurishaji waangamizwa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i11137-makumi_ya_magaidi_wakufurishaji_waangamizwa_syria
Makumi ya magaidi wakufurishaji wameangamizwa katika mashambulizi ya jeshi la serikali ya Syria kwa kushirikiana na wapiganaji wa muqawama katika mkoa wa Aleppo, kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 13, 2016 04:37 UTC
  • Makumi ya magaidi wakufurishaji waangamizwa Syria

Makumi ya magaidi wakufurishaji wameangamizwa katika mashambulizi ya jeshi la serikali ya Syria kwa kushirikiana na wapiganaji wa muqawama katika mkoa wa Aleppo, kaskazini mwa nchi hiyo.

Sanjari na jeshi la serikali kuendelea kusonga mbele katika viunga vya kaskazini mwa mkoa huo, magaidi wanaokaribia 100 wameangamizwa katika operesheni hizo za jeshi la Syria. Katika operesheni hizo jeshi la Syria limedhibiti eneo la Al-Lirmun kaskazini mwa mkoa huo. Kadhalika wanamgambo wa muqawama wamefanikiwa kuvunja mstari wa kujihami wa magaidi katika eneo la kambi ya Handarat na hivyo kudhibiti kikamilifu maeneo ya Madajin na al Karum.

Wakati huo huo Jeshi la Anga la Syria limefanya mashambulizi makubwa dhidi ya ngome za makundi ya kigaidi katika barabara ya al Castello na maeneo ya mashamba ya al-Mallah kusini, mashambulizi ambayo yangali yanaendelea.

Katika fremu hiyo, juhudi za magaidi za kujaribu kudhibiti tena maeneo yaliyotwaliwa na jeshi la serikali ya Syria zimegonga mwamba. Mbali na hayo ndege za kivita za Syria zimeshambulia msafara wa magari wa magaidi katika maeneo ya Mariyah, al Tharah, al-Jafra katika mji wa Deir ez-Zor.