Jun 13, 2024 07:20 UTC
  • Mashambulio makubwa zaidi ya kulipiza kisasi ya Hizbullah dhidi ya Israel

Shambulio kubwa zaidi kuwahi kufanywa na Hizbullah ya Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba iliyopita hadi sasa limepelekea kengele ya hatari kupigwa katika vitongoji zaidi ya 60 vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Hizbullah imetangaza kuwa shambulio lake la jana Jumatano ndilo shambulio kali zaidi kuwahi kufanywa na harakati hiyo tangu kumalizika Vita vya Pili vya Lebanon katika majira ya joto ya mwaka 2006. Awali Hizbullah ilitangaza kuuawa shahidi wapiganaji wake wanne akiwemo kamanda wa kijeshi katika shambulio la utawala wa Kizayuni katika mji wa Jouaiya kusini mwa Lebanon ambapo, Talib Sami Abdullah kwa lakabu ya Haj Abu Talib, mmoja wa makamanda wake wa ngazi za juu, aliuawa shahidi katika shambulio hilo.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz liliandika kuwa Hizbullah ilirusha makombora 200 kutoka kusini mwa Lebanon kuelekea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel. Wazayuni wamesema shambulio hilo kubwa na lisilo na mfano wake la Hizbullah mbali na kusababisha hasara kubwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni pia limesababisha moto mkubwa katika maeneo mengi ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Shirika rasmi la radio na televisheni ya utawala wa Kizayuni (KAN) limenukuu vyanzo vya habari vya kuaminika vikisema kwamba utawala huo umeiomba Marekani iusaidie kukabiliana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za harakati ya Hizbullah.

Amichai Stein, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa shirika hilo amedokeza kuwa ili kujaribu kuonyesha kuwa Marekani iko upande wa Israel katika mzozo wake wa hivi sasa huko Lebanon, watawala wa Israel wameomba msaada wa nchi hiyo kwa lengo la kuishinikiza Hizbollah isifanye operesheni kubwa za kijeshi dhidi ya utawala huo haramu. Katika miezi michache iliyopita na kufuatia jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika eneo hilo, Hizbullah ya Lebanon imekuwa ikishambulia maeneo ya kijeshi ya utawala huo ghasibu kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, suala ambalo limeibua hofu kubwa miongoni mwa walowezi wa Kizayuni katika maeneo hayo. Kufikia sasa makumi ya maelfu ya Wazayuni wamekimbia vitongoji vyao karibu na mpaka wa Lebanon kwa kuhofia mashambulizi ya Hizbullah.

Hizbullah yalenga mareneo nyeti ya kiulinzi ya utawala wa Kzayuni

Kwa kuzingatia ushahidi uliopo, mashambulio ya Hizbullah ambayo yanajumuisha silaha mpya na za hali ya juu zaidi dhidi ya utawala wa Kizayuni yameshadidi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, ambapo utawala huo umeanzisha mashambulio yake huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza. Licha ya changamoto nyingi ambazo utawala wa Kizayuni unakabiliana nazo katika eneo la kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ndege zisizo na rubani za Hizbullah zimekuwa jinamizi kubwa zaidi kwa utawala huo ghasibu katika miezi michache iliyopita, ambapo wavamizi hao wanaona kuwa ni changamoto isiyoweza kupatiwa ufumbuzi kwa haraka na ambayo imeharibu kabisa "ubora wa ulinzi wa anga wa Israel." Kudunguliwa mara kwa mara ndege zisizo na rubani za jeshi la Kizayuni na Hizbullah na kuendelea kufanikiwa operesheni za ndege zisizo na rubani za muqawama wa Lebanon dhidi ya maeneo ya maadui wanaoikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina ni mshtuko mkubwa kwa watawala na idara za kijasusi za Israel.

Vyombo vya habari vya Kiibrania vimeripoti kwamba tangu kuanza mapigano kati ya Hizbullah na jeshi la Israel katika kipindi cha miezi minane iliyopita, takriban roketi 17,000 zimerushwa dhidi ya Israel, ambapo roketi 3,000 zilitokea upande wa Lebanon na kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo yenye stratijia kubwa ya Israel.

Hii ni pamoja na ukweli kwamba katika kipindi cha miezi 8 iliyopita, Hizbullah bado haijatumia makombora yake yenye kulenga shabaha bila kukosea, makombora ambayo yanaweza kubeba hadi tani moja ya mada za milipuko. Hizbullah bado haijafichua kikamilifu vikosi vyake vya ndege zisizo na rubani, hasa ndege zisizo na rubani za kujilipua, bali imetosheka tu kwa kurusha droni 2 hadi 3 wakati mmoja. Aidha, Hizbullah bado haijafanya mashambulio makubwa ya kurusha mamia ya makombora kwa wakati mmoja dhidi ya  Israel, mahambulio ambayo yanalemaza pakubwa mfumo wa ulinzi wa anga wa Iron Dome. Maafisa wa jeshi la Israel wana wasiwasi mkubwa kuhusu makombora ya kulenga shabaha bila kukosea ya Hizbullah, kwa sababu wanajua vizuri kwamba Hizbullah itatumia makombora hayo kwa kiwango kikubwa katika makabiliano yoyote ya kijeshi kwa lengo la kuharibu mifumo ya ulinzi wa anga ya jeshi la Israel, ili iweze kufanya mashambulizi makubwa katika maeneo ya ndani kabisa ya Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu).

Aina moja ya droni za Israel zinazotunguliwa mara kwa mara na Hizbullah

Kwa mujibu wa tathmini ya taasisi za usalama na kijeshi za Israeli, ikiwa mzozo wa upande wa kaskazini utaongezeka kwa kiwango kikubwa, Hizbullah inaweza kurusha makombora kati ya 3,000 na 5,000 kwa siku kuelekea Israeli (Palestina inayokaliwa kwa mabavu) ambapo asilimia 90 ya makombora hayo yatafika takriban umbali wa kilomita 40 kutoka mpaka wa Lebanon na makombora yaliyosalia yatarushwa kuelekea katikati mwa Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu). Hii ina maana kwamba vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye mpaka huo hadi maeneo ya mji wa Haifa vitakabiliwa na uharibifu mkubwa zaidi.

Makadirio ya duru za Wazayuni yanaonyesha kuwa, kadiri Israel itakavyoamua kuongeza mashambulio yake dhidi ya Gaza, ndivyo hali ya upande wa kaskazini nayo itazidi kuwa ya wasiwasi, ambapo Hizbullah itaongeza operesheni zake kwa kasi, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa harakati hiyo ya muqawama kuzindua silaha zake mpya ambazo bila shaka zitawashtua Wazayuni watenda jinai. Kuna uwezekano pia kwamba Netanyahu na wajumbe wengine wa baraza lake la mawaziri wenye itikadi kali watazidisha vita kusini mwa Lebanon kutokana na kuongezeka mashinikizo ya kimataifa ya kuwataka wasitishe vita vyao vya jinai huko Gaza, ili kuandaa mazingira mazuri ya kuzuia mashtaka ya jinai za kivita dhidi yao kuhusu na wakati huo huo kuzuia kuanza tena wimbi la migawanyiko ya ndani ya Israel baada ya kumalizika vita vya Gaza.